Waraka uliotolewa na Umoja wa Mataifa unaishutumu serikali ya Sudan
Kusini kuwapa mafunzo ya kijeshi watoto wadogo wiki iliyopita,
ikijitayarisha kwa uwezekano wa mapigano mapya.
Waraka, ambao shirika la habari la Associated Press limeupata, unasema
kuwa mwanasiasa mmoja wa ngazi za juu aliyeteuliwa na Rais Salva Kiir wa
Sudan Kusini ndiye aliyeongoza mafunzo hayo ya kijeshi kwa wavulana wa
kijiji kizima, huku akitumia vitisho, kwa wale wanaokataa. Kwa mujibu wa
waraka huo, miongoni mwa wavulana hao walioorodheshwa kujiunga na
mapigano, wamo wenye umri wa hadi miaka 12.Hata hivyo, msemaji wa jeshi la serikali, Lul Ruai Koang, amekanusha taarifa hizo, na badala yake akasema vijana wote wanaojiunga na jeshi huwa hawalazimishwi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizomo kwenye waraka huo, uingizaji wa watoto jeshini ulianza muda mchache baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kutuma wanajeshi wengine 4,000 wa kulinda amani katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ili kuwalinda raia, kufuatia kuanza upya kwa mapigano katika mji mkuu, Juba, mwezi uliopita.
Tabia ya makundi hasimu kutumia watoto kama wapiganaji kwenye mapambano yao, imekuwepo kwa muda mrefu kwenye taifa hilo jipya kabisa barani Afrika.
Umoja wa Mataifa unasema watoto 650 wamejiunga na makundi yenye silaha nchini Sudan Kusini mwaka huu pekee. Kiasi cha watoto 16,000 wameingizwa kwenye makundi hayo tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanza Disemba mwaka 2013. source DW
Post a Comment