GARI la Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe, limekamatwa na
kuendelea kushikiliwa mjini
Mombasa nchini Kenya, kutokana
na kuwa na namba mbili.
Taarifa kutoka Kenya zilizolifikia
gazeti hili jana, zilieleza kuwa
polisi nchini Kenya walipata taarifa
za kuwepo kwa gari hilo na watu
ambao walionekana kutokuwa na
kazi maalumu.
Baada ya kupata taarifa hizo,
Polisi hao walio katika msako wa
wageni na magari yanayotiliwa
shaka kuhusika katika uhalifu na
ugaidi, walianza kulifuatilia na
kubaini wahusika wa gari hilo.
Ufuatiliaji huo kwa mujibu wa
taarifa hizo, ulibaini wahusika wa
gari hilo walipofika Mombasa
kutokea Tanzania, hawakuonekana
kupokewa na mwenyeji yeyote,
hali inayomaanisha wenyewe ni
wenyeji wa mji huo.
Taarifa za Polisi zilibainisha kuwa
uchunguzi wao ulibaini kuwa gari
hilo liliwabeba Mbowe, Mbunge wa
Mwanza Mjini, Ezekiah Wenje na
dereva Ibrahim Nguzo.
Polisi hao inadaiwa walitilia shaka
gari hilo kutokana na kuwa na
namba za usajili STK 8146,
ambazo zilipandishiwa juu ya
nambari halisi za gari hilo ambazo
ni KUB.
Uchunguzi wa Polisi hao ulibaini
kuwa Mbowe na Wenje waliwasili
Mombasa, Kenya kwa gari
wakitokea Tanzania kupitia mpaka
wa Horohoro/Lungalunga na
kwenda moja kwa moja hotelini.
Mashaka kwa Polisi hao
yaliongezeka baada ya Mbowe na
Wenje Aprili 26 mwaka huu
kusafiri kwenda Nairobi kwa
ndege, na kumwacha dereva
pamoja na gari hotelini.
Kutokana na hali hiyo, Jumatatu
wiki hii saa 5.00 asubuhi askari
Polisi wa Mombasa walimkamata
Ibrahim pamoja na gari hilo, baada
ya kuonekana amekaa hotelini
muda mrefu bila ya shughuli
zozote.
“Hapo ndipo alipotoa habari
kwamba alikuwa akiwasubiri
wakubwa zake ambao walikwenda
Nairobi tangu Aprili 26 na
hawakuwa wamerejea,” ilieleza
taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,
Ibrahim alipoulizwa kwa nini gari
lilikuwa na nambari za
kupandishiwa, alijibu huo ulikuwa
ni uamuzi wa bosi wake Mbowe.
Polisi hao waliamua kukamata gari
hilo na kulipeleka katika kituo cha
Polisi cha Kati kwa mahojiano
zaidi na baada ya mahojiano,
aliachiliwa Ibrahim huru lakini gari
limeendelea kuzuiliwa kituoni hadi
Mbowe na Wenje watakapofika
kwa ajili ya kuhojiwa.
Gazeti hili lilimtafuta msemaji wa
Chadema, Tumaini Makene,
ambaye aliomba muda kupata
taarifa halisi za tukio hilo na
baadaye alituma ujumbe mfupi wa
maneno ambao hakukanusha wala
kukubali kutokea kwa tukio hilo.
“Suala hilo ni la kiutawala
napendekeza utafute uongozi wa
Bunge…mtafute Katibu wa Bunge
(Dk Thomas Kashililah), bila shaka
ataweza kukueleza juu ya safari
ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni na mengine yote ya
kiutawala unayotaka kupata
majibu yake,” alieleza Makene.
Gazeti hili lilimtafuta Mbowe,
Wenje na Kashililah lakini simu
zao hazikupatikana.
Post a Comment