WALIMU WAPIGWA MAWE NA WANAFUNZI WA SHULE YA MIZENGO PINDA KWA MADAI KUWA NI WACHAWI

WALIMU WAPIGWA MAWE NA WANAFUNZI WA SHULE YA MIZENGO PINDA KWA MADAI KUWA NI WACHAWI

 
WANAFUNZI wa shule ya sekondari ya Mizengo Pinda  kata ya Kibaoni  Wilayani Mlele mkoani Katavi, wamemshambulia kwa mawe na matofali mkuu wa shule hiyo na mwalimu wa taaluma na kuharibu jengo la utawala na nyumba za walimu hao baada ya kuwatuhumu walimu hao kuwa ni washirikina.

Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa katavi, Joseph Myovela, alisema tukio hilo limetokea juzi saa 2:30 usiku shuleni hapo baada ya kuzuka kwa tafrani iliyodumu kwa zaidi ya saa 1:30.

Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa chanzo cha tukio hilo kilitokana na mwanafunzi mmoja aitwaye Jofley Pinda kushikwa na ugonjwa wa mapepo uliomfanya aanguke chini ambapo tukio hilo lilitokea mchana wa saa saba.

Alisema wakati akiwa ameshikwa na mapepo hayo aliwataja Alico Kamyoge (36) ambaye ni Mkuu wa shule hiyo ya sekondari ya Mizengo Pinda na mwalimu wa taaluma Bonifasi Nsalamba (35) kuwa ndio wamemroga ugonjwa huu wa mapepo

Myovela alisema  ilipotimia muda huo wa saa mbili wanafunzi hao walijikusanya na kuandamana hadi kwenye jengo la utawala na kuanza kulishambulia kwa mawe na matofali na kuvunja mlango na dirisha la jengo hilo.

Alieleza baada ya kufanya uharibifu kwenye jengo la utawala walielekea kwenye ofisi ya mwalimu wa taaluma ambapo waliharibu mtandao wa mawasiliano kwenye Computer.

Wanafunzi hao ambao muda wote walikuwa na hasira walielekea nyumbani kwa mkuu wa shule, huku wakiwa na matofali na mawe walipofika na kumkosa mkuu washule aliyekuwa amekwenda kwenye matembezi ya jioni walianza kushambulia nyumba yake kwa mawe na tofali na kuharibu mlango na madirisha.

Kaimu kamanda Myovela alisema  kundi hilo lilielekea nyumbani kwa mwalimu wao wa taaluma Bonifasi Nsalamba ambapo walimkuta akiwa anajiandaa kuingia ndani ya nyumba yake akitokea matembezini.

Ndipo walipoanza kumshambulia kwa mawe katika sehemu mbalimbali za mwili wake huku wakimzomea kuwa mchawi huyo mshirikina ..


Alisema katika shambulio hilo wanafunzi walimjeruhi mwalimu Bonifasi na kumsababishia majeraha katika mwili wake na aliweza kutibiwa katika zahanati ya kibaoni na kuruhusiwa na hali yake inaendelea vizuri.

Jeshi la polisi mkoa wa katavi limetoa wito kwa wanafunzi wa shule hiyo na shule nyingine  za mkoa huo waachane na kuamini imani za ushirikina na polisi inaendelea na uchunguzi  wa tukio hilo ili kuwabaini waliohusika na
waweze kuchukuliwa hatua.

Post a Comment

Contact Form

Name

Email *

Message *

designed by izack. Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget