TAMKO LA THRD-COALITION KUHUSU KUJERUHIWA KWA SHEIKH ISSA PONDA ISSA...

PONDA 58e9b
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI 12 AUGUSTI 2013
YAH: KUJERUHIWA KWA SHEIKH ISSA PONDA ISSA
KWA mara nyingine tena, sisi mashirika ya utetezi wa haki za binadamu, THRD-Coalition, LHRC, SIKIKA, TGNP, CPW na TAMWA tumewaiteni hapa kuwaomba mtufikishie ujumbe wetu huu kwa wananchi wa Tanzania. Ujumbe wenyewe unahusu kujeruhiwa kwa Sheikh Issa Ponda Issa na hali inayoendelea kukua ya uvunjaji wa haki za binadamu nchini.
Jana, tarehe 11 August 2013 tulipokea kwa masikitiko makubwa taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi nchini kuhusu tukio la kujeruhiwa kwa Katibu wa Jumuiya za Kiislam Tanzania – Sheikh Issa Ponda Issa lililotokea mkoani Morogoro tarehe 10 August 2013.
Awali ya yote, tuseme wazi, kuwa hatufungamani na taasisi yoyote ya dini wala chama chochote cha siasa. Wajibu wetu mkuu ni kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaheshimiwa na kulindwa kikamilifu bila upendeleo au ubaguzi kwa misingi yoyote ile.
Tunasikitishwa sana na hali ya uvunjaji wa haki za binadamu inayotokana na tabia iliyokithiri ya vyombo vya dola kutumia nguvu inayokiuka haki za msingi za wananchi. Tunapenda kuwafahamisha kuwa, tunalaani matumizi ya nguvu yanayofanywa na vyombo hivyo. Pia, tunahuzunishwa na uhalifu, vurugu na tabia ya wananchi kujichukulia sheria mikononi na hatukubaliani na vitendo vyovyote vile vya kuvunja amani. Maathalan vitendo vinavyoongezeka vya wananchi kutumia tindikali kama silaha dhidi ya wenzao.
Tunafahamu kuwa, wajibu wa Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao na kuwa wanayo haki ya kuwakamata washukiwa wa uahlifu kwa mujibu wa sheria. Pamoja na yote tunalaani kitendo alichofanyiwa Kiongozi wa Jumuiya za Kiislam Tanzania, Sheikh Issa Ponda Issa. Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, tumeelezwa kuwa Sheikh Ponda alijeruhiwa wakati 'polisi walipopiga risasi hewani ili kuwatawanya wale waliokuwa wafuasi wake.' Na pia kwa mujibu wa vyombo vya habari vilivyodai kumhoji ndugu Isihaka Rashid, tumeelezwa kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi begani na Polisi.
Kutokana na hali hiyo, sisi watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia:
1. Kutokana na uzoefu tulio nao wa matukio yanayofanana ya hayo, hatuna imani kabisa na kamati/tume iliyoteuliwa na Jeshi la Polisi ili kuchunguza tukio hilo. Hofu yetu inatokana na ukweli kwa Jeshi hilo ndilo linalotuhumiwa kumjeruhi Sheikh Ponda, na kutokana na misingi ya haki za asili – haikubaliki mhusika kuwa hakimu kwenye shauri linalomhusu.
2. Tunalaani kabisa utaratibu ambao Jeshi la Polisi liliutumia ili kumkamata Sheikh Ponda. Utaratibu huu wa kumkamata mtuhumiwa mbele ya halaiki ya wafuasi wake ulikuwa ni hatarishi kwa maisha ya askari wenyewe pamoja na maisha ya raia na pia ilikuwa inaibua hamasa na hamaki ya umma.
3. Tunatoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo Kikatiba ina jukumu la kufuatilia na kuchukua hatu kwa masuala kama haya , ifanye hima kufuatilai na kuchukua hatua zote stahiki za kisheria. Aidha ikiwa Tume itahitaji msaada wetu wa rasilimali watu na fedha, tuko tayari kuisaidia ili ifanye kazi hii kwa haraka kama inavyostahili.
4. Tunaiomba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ifuatilie pia matukio mengine ya matumizi ya nguvu yanayofanywa na vyombo vya dola katika sehemu mbalimbali kama vile Mtwara, Arusha, Zanzibar, Kigoma na sehemu nyinginezo nchini.
5. Tunawaomba wananchi wawe watulivu na wazingatie sheria za nchi katika kudai haki zao.
6. Tunavitaka vyombo vya dola vianza kujifunza kutenda haki kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora.
7. Tunampa pole katibu wa Jumuiya za Kisilam Tanzania Sheikh, Issa Ponda Issa pamoja na wote walioathirika katika kadhia hiyo.
Imeandaliwa na Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu Tanzania na kusoma kwenu kwenu na;
Onesmo Olenguruwa,
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania.

Post a Comment

Contact Form

Name

Email *

Message *

designed by izack. Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget