Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,Freeman Mbowe akizungumza kwenye
kikao cha maamuzi ya pamoja na Vyama vingine juu ya kususia mjadala wa
Marerkebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Bungeni juzi
jioni.Kushoto ni Mbunge wa Mkanyageni,Habib Mnyaa(CUF)na Mbunge wa
Kuteuliwa NCCR Mageuzi,James Mbatia.Picha na Fidelis Feli
Maoni ya
Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu Muswada wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba wa 2013 yanadaiwa kuwa yalibadilishwa dakika za
mwisho na kwamba suala hilo ndicho kiini cha vurugu zilizotokea bungeni
mjini Dodoma juzi.
Gazet la
mwananchi limefanikiwa kuona nakala inayodaiwa kuwa ni maoni ya awali
ya kamati hiyo ambayo yalikuwa na mapendekezo yanayotaka kuwapo kwa
marekebisho kadhaa kwenye muswada huo, tofauti na yale yaliyowasilishwa
bungeni juzi na Mwenyekiti wa Kamati, Pindi Chana.
hdg
Jumatano
na Alhamisi wiki hii kulikuwa na mvutano mkubwa bungeni kiasi cha
wabunge wa upinzani kutoka vyama vitatu vya NCCR -Mageuzi, Chadema na
CUF kuungana na kususia mjadala kuhusu muswada huo.
Imedokezwa
kuwa mvutano mkali kuhusu muswada huo ulianza ndani ya kamati hiyo
wakati wajumbe wake ambao ni wabunge wa CCM walipotumia wingi wao
kubadili maoni ya awali na kuweka maoni mapya, hatua ambayo inadaiwa
kuwa ilikuwa na msukumo wa Serikali nyuma yake.
Ndani ya
Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, wabunge wa upinzani ambao
kwa idadi yao ni wachache walishindwa kuzuia mabadiliko hayo ya "lala
salama" yanayodaiwa kuwa yaliwekwa Septemba 2, mwaka huu, hivyo
waliazimia kuhamasisha wabunge wote wa upinzani kupinga marekebisho hayo
kutokana na sababu kuu mbili.
Sababu
hizo ni kutofanyika kwa mikutano ya wazi kwa umma (public hearing)
upande wa Zanzibar na hatua ya kuwapo kwa mapendekezo ya Rais
kurundikiwa madaraka makubwa ya uteuzi wa wabunge kutoka asasi za
kijamii watakaoingia katika Bunge la Katiba.
Habari
zinasema wakati fulani Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alitembelea
kamati hiyo wakati ikiedelea na vikao vyake na kukuta mvutano mkali
kuhusu suala la marekebisho ya sheria ya sheria hiyo na alishauri kwamba
pale ambapo hawataweza kuelewana basi wasubiri uamuzi ndani ya Bunge.
Jana
gazeti hili lilimtafuta Chana kupitia simu yake ya mkononi na baada ya
kumweleza kuhusu madai hayo alisema: "Tafadhali sana kwa sasa niko
kwenye kikao, kwanza simu yako nimeipokea kwa heshima tu, tutafutane
wakati mwingine".
Waziri wa
Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alikiri kwamba kulikuwa na
mapendekezo ya kuongeza idadi ya wabunge na namna ya kuwapata, lakini
Serikali iliyakataa katika hatua ya majadiliano kabla ya suala hilo
kufikishwa bungeni.
Tofauti ya maoni
Nakala ya
taarifa ya awali ilipendekezwa kuwa katika kuteua wajumbe 166 wa Bunge
la Katiba, Rais azingatie kikamilifu mtiririko wa mapendekezo ya kila
kundi lililoainishwa katika kifungu cha (1) (c).
"Na
endapo Rais hatazingatia mapendekezo ya kundi mojawapo, Rais afanye
mrejesho kwa taarifa kwa kundi husika juu ya sababu za kutozingatia
mtiririko wa mapendekezo yaliyowasilishwa kwake," inasema taarifa
hiyo.Taarifa hiyo inaongeza kuwa kamati hiyo ilikuwa na maoni kwamba
makundi mengine ya kijamii yaongezwe katika kifungu cha 22(1) (c) cha
sheria mama, ili kupanua wigo wa uwakilishi mpana katika Bunge la
Katiba, hivyo kuongeza idadi ya wabunge hao kutoka idadi ya awali 166
hadi kufikia 201.
"Kamati
inashauri kuwa idadi ya wajumbe iwe 201 badala ya idadi ya wajumbe 166
iliyotajwa katika sheria mama, ili kupata idadi ya wajumbe watakaounda
Bunge Maalumu la Katiba," inasomeka taarifa hiyo.
Hata
hivyo, maoni hayo yanatofautiana na yale yaliyowasilishwa bungeni juzi
na jana, kwani yanaonyesha kwamba kulikuwa na majadiliano na mashauriano
baina ya kamati na Serikali, hivyo ilikubaliana kuwa "Rais apewe
mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe Bunge la Katiba" huku idadi ya
wabunge wa kuteuliwa wakibaki 166.
Kifungu
hicho kiliondoa haki ya kila taasisi kuteua jina la mjumbe wake katika
Bunge hilo na badala yake, ikapendekezwa kuwa Rais atapelekewa matatu
ili ateue moja kati ya hayo.
Hata
hivyo, jana wakati Bunge lilipoketi kama kamati kwa ajili ya kupitia
vifungu vya marekebisho ya muswada huo, Serikali iliwasilisha
marekebisho ya nyongeza ambayo yanazitaka asasi za kiraia ziteue majina
tisa na kati ya hayo Rais anaweza kuteua jina moja na kama asiporidhika
anaweza kuteua mtu kutoka nje ya orodha hiyo.
Kuhusu
suala hilo Chikawe alisema: "Tangu awali ilikuwa inaonyesha wajumbe ni
166. Ni kweli Kamati ilipendekeza wajumbe hao waongezeke hadi 201 lakini
pendekezo hilo halikukubaliwa, ikabakia wajumbe watakuwa 166."
Ushiriki wa Zanzibar
Itakumbukwa
kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilipewa wiki nne za kuendesha
vikao vyake kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika
jana, tofauti na kamati nyingine ambazo zilipewa wiki mbili.
Baadhi ya
wabunge (hasa wa upinzani) wanasema madhumuni ya kupewa muda huo ni
kama hayakutimia kwani hawakuweza kupokea maoni kutoka kwa makundi
muhimu hasa ya upande wa Zanzibar kama ilivyokusudiwa.
Hata
hivyo, jana Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ), Balozi Seif Ali Idd, alilihakikishia Bunge kuwa upande wa
Zanzibar ulishirikishwa katika kutoa maoni ya muswada huo.
Hatua ya
Balozi Idd kutoa ufafanuzi ilitokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa
Sikonge, Said Nkumba(CCM) aliyeomba kwa vile Balozi Seif yuko ndani ya
Bunge basi apewe fursa kufafanua utata huo.
Kauli ya
Balozi Idd inapingana na ile iliyotolewa juzi jioni na Mnadhimu wa Kambi
ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye alisema ni kosa kubwa kamati
kutochukua maoni ya Wazanzibar.Lissu alisema kulikuwa na njama tangu
mwanzo za kuhakikisha kuwa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
haichukui maoni ya Wazanzibari na hilo linathibitishwa na ratiba
zilizokuwa zimeandaliwa na kamati.
"Katika
orodha ya wadau wote 22 waliokuwa wameorodheshwa katika kutoa maoni yao
juu ya muswada huu hakukuwa na Mzanzibari hata mmoja...tulipoipitia
tukasema hapana Wazanzibari wako wapi," alisema.
Lissu
alisema yeye, Mwenyekiti wa Kamati, Chana na Makamu Mwenyekiti, William
Ngeleja walikwenda kumwona Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah na
kumweleza azma yao ya kwenda kuzungumza na wadau wa Zanzibar.
"Katibu
akatwambia kwamba yeye ana fedha za kutuwezesha kukaa Zanzibar hata wiki
moja, kwa hiyo tukarudi kwenye kamati tukatengeneza ratiba mpya na
tukaongeza wadau sita wa Tanganyika na Wazanzibari wanane," alisema
Lissu.
Aliwataja
wadau hao kuwa ni Chuo cha Taifa Zanzibar, Chuo Kikuu cha Zanzibar,
Chama cha Mawakili Zanzibar, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar,
Chama cha Walemavu Zanzibar na Profesa Abdul Shariff.
Wadau
wengine walikuwa ni Shirikisho la Vyama visivyo vya Kiserikali Zanzibar
(Angoza) na Jumuiya ya Misikiti Zanzibar na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar,
lakini hatukuwahi kukutana nao na kupokea maoni yao.
"Tukakubaliana
kuwa tutakaa Zanzibar kwa siku tatu kuanzia Julai 14 hadi Julai 16
mpaka leo hatujawahi kuambiwa kwa nini tulizuiwa kwenda Zanzibar, lakini
maneno yaliyokuwa yakisikika eti kwa sababu za kiusalama," alisema.
Lissu
alisema wakati kamati yao ikiambiwa haiwezi kwenda Zanzibar kwa sababu
za kiusalama, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge hilo ilikuwa Pemba
ikiendelea na ziara zake.CHANZO MWANANCHI.
Post a Comment