MTANGAZAJI maarufu ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mlimani, Dar na Mshereheshaji (MC), Godwin Gondwe ‘Double G’ wikiendi iliyopita alimwaga machozi hadharani wakati akitoa ushuhuda wa maisha aliyopitia wakati wa semina ya ujasiriamali inayofanyika kila Jumapili katika Ukumbi wa Kituo cha Mafuta cha Victoria, kilichopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo ambalo huratibiwa na kikundi cha Kusifu na Kuabudu cha Glorious Worship Team (GWT), Gondwe alisema anashangazwa na hatua aliyofikia katika maisha yake, kwani aliishi kwa taabu na kufanya kazi ambazo wakati mwingine zilihatarisha afya yake, lakini kwa uwezo wa Mungu, amevuka na sasa anamshukuru.
Akiwa katika hisia kali, Gondwe alitokwa na machozi wakati akikumbuka maisha aliyopitia na kuwaambia mamia ya watu waliohudhuria semina hiyo kuwa anahisi uwepo wa Mungu ndani yake na kwamba machozi anayotoa ni mapokeo na sifa kwa Muumba juu ya yote aliyomtendea hadi sasa.
“Nimetoka kwenye familia ya kawaida sana, maisha yangu yamejaa mihangaiko na shuhuda nyingi ngumu, lakini kubwa ni kufanya kazi ya kutunza choo katika hospitali ya wagonjwa wa kifua, tena bila mipira (gloves), jambo lililohatarisha sana afya yangu,” alisema mtangazaji huyo na kuongeza;
“Pia, niliwahi kuwa mhudumu wa hoteli, yote hayo ni kule Mwanza, kwa hiyo kufika hapa ni kwa neema ya Mungu tu, nawaomba watu wasikate tamaa, wasikubaliane na hukumu ya binadamu na wala mazingira yasiwaamulie hatima yao, waseme I’m what God says I’m (Niko hivi nilivyo kutokana na jinsi Mungu anavyotaka).
“Pia, tusisahau kumshukuru Mungu kwa kumtolea, maana anasema nijaribuni kwa matoleo, yaani leo hii niko hapa! Hakika huyu ni Mungu, kila kitu kinawezekana,” alisema Gondwe na kuwataka watu kutomsahau Mungu kwa kumtolea kwa kila mafanikio wanayofikia, kwani ndiyo siri kubwa ya maisha.
Mbali na mtangazaji huyo, pia mwalimu mahiri nchini wa kuhamasisha watu kujikomboa na umaskini, Eric Shigongo alitoa somo la jinsi ambavyo mke, mume au mchumba wanavyoathiri maisha yetu, somo ambalo litaendelea wiki hii.