Wahamiaji 6,500 wameokolewa nje ya pwani ya Libya hapo jana kupitia
operesheni 40 tofauti za uokozi. Ni idadi kubwa ya wahamiaji
walionusurika, katika safari za hatari za kuingia Ulaya katika siku za
hivi karibuni.
Kikosi cha ulinzi wa pwani kimeandika katika ukurasa wao wa Twitter,
kwamba uokoaji huo wa wahamiaji 6,500 uliwezekana kupitia operesheni 40
tofauti, zilizojumuisha meli za Kitaliana, mashirika ya kibinaadamu
pamoja na Shirika la Kulinda Mipaka ya Umoja wa Ulaya Frontex.Picha za kushtusha za moja ya operesheni hizo za uokoaji, zinawaonyesha wahamiaji wapatao 700 wamekusanyika katika boti ya kuvulia, huku wengine wakioneka wanajitosa kutoka katika boti hiyo wakiwa wamevalia makoti ya kuokoa maisha, wakijaribu kuogelea ili wawafikie waokoaji.
Mtoto mwenye umri wa siku tano alikuwani miongoni mwa wahamiaji waliokolewa pamoja na watoto wachanga wengine, ambao walibebwa juu kwa juu kwa kutumia helikota ya uokozi na haraka kufikishwa hospitali moja nchini Italia, hayo ni kwa mujibu wa Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), ambao walishiriki katika operesheni hizo za uokozi.
Siku ya Jumapili pekee, zaidi ya wahamiaji 1,100 waliokolewa wote katika eneo moja.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa pamoja na wanajeshi wa majini, idadi jumla ya wahamiaji waliowasili nchini Italia hadi sasa imeshatimia 112,500, ikiwa imepungua kidogo ikilinganishwa na ya mwaka uliopita ambayo ilifika wahamiaji 116,000 katika wakati kama huu.
Wengi wa wahamiaji wanatokea Afrika
Karibu wahamiaji wote miongoni mwa hao, wametokea nchi za Afrika Magharibi pamoja na za Pembe ya Afrika.
Kawaida wahamiaji hao huondokea nchini Libya, wakati bahari ikiwa shwari huku boti zikitegemea upepo wa kusini kuzisukuma katika bahari ya kimataifa.
Waokoaji wa kikosi cha Italia wametabiri kwamba kuboreka kwa hali ya hewa, kutawahamasisha zaidi wahamiaji kufunga safari za hatari za kuvuka bahari ya Mediterania.
Boti zinazotumika kwa safari hizo mara nyingi zinakuwa dhaifu, haziwezi kubeba idadi kubwa ya watu wanaojazwa ndani yake. Pamoja na hayo, baadhi ya wahamiaji huanza safari hiyo wakiwa hawana afya nzuri na hivyo hushindwa kuhimili safari za aina hiyo hata pale bahari inapokuwa imetulia.
Tokea mwaka huu ulipoanza zaidi ya wahamiaji 3,000 wamepoteza maisha wakiwa majini wakijaribu kuelekea nchini Ugiriki au Italia. Hilo ni ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka jana katika wakati kama wa sasa.
Wahamiaji wengine 204,000 wamevuka bahari ya Mediterania na kuingia barani Ulaya katika miezi ya sita ya kwanza ya mwaka huu.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema bara la Ulaya linakabiliana na mgogoro mkubwa wa wahamiaji kuwahi kutokea tangu vita vikuu vya pili vya dunia.source DW
Post a Comment