
HII NI MAKALA NZIMA YA KUHUSU MATOKEO NA TAMKO RASMI LA CHADEMA
NA JISI WANNACHI WANAVYOSEMAA
MATOKEO KIDATO CHA IV VILIO KILA KONA
CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa muda wa siku 14 Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, na Naibu wake, Philip
Mulugo, kuhakikisha wamejiuzulu nyadhifa zao.
Kauli hiyo
ya CHADEMA imetolewa na mwenyekiti wake taifa, Freeman Mbowe, wakati
alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara, uliofanyika jana katika
viwanja vya Furahisha Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ikiwa ni
ufunguzi wa Baraza la Viongozi wa CHADEMA, Kanda ya Ziwa Magharibi.
Mbowe ambaye
aliongoza maandamano makubwa ya magari na pikipiki kuelekea uwanjani
hapo, alisema, Kawambwa, naibu wake, Mulugo, pamoja na katibu mkuu wa
wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa
sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika
mitihani ya kuingia kidato cha kwanza.
Alisema
waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya
na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za
msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Mbowe
alisema hili ni janga la kitaifa, hivyo lazima Kawambwa aondoke ndani ya
wiki mbili, vinginevyo CHADEMA itaitisha maandamano makubwa nchi nzima
kushinikiza kiongozi huyo ang’oke madarakani.
“Kwa vile
Kawambwa ameshindwa kuisimamia vema sekta hii ya elimu na kwa vile
watoto wetu wengi wanafeli na kuishia kuandika matusi kwenye mitihani
yao, CHADEMA tunampa wiki mbili awe amejiuzulu.
“Kila mwaka
wanafunzi 1,200,000 hadi 1,300,000 nchi nzima wanafanya mitihani yao.
Lakini wanaoshinda ni kati ya 35,000 hadi 400,000 pekee, hivyo watoto
wengine wanashindwa kuendelea na masomo yao. Kwa hiyo tunataka huyu
waziri na naibu wake wajiuzulu ndani ya wiki mbili,” alisema Mbowe.
Alisema, kwa
sasa Tanzania inazalisha vijana wapatao 800,000 kwa mwaka ambao
wanakosa fursa ya kuendelea na masomo yao na alimtaka Rais Jakaya
Kikwete kuacha kucheka na kubembeleza viongozi wabovu wanaodidimiza
maendeleo ya nchi na raia wake na kwamba Tanzania inakabiliwa na majanga
makubwa mawili ya elimu duni na udini.
Kuhusu Bunge
kutoonyeshwa ‘live’, Mbowe alimuonya Spika Anna Makinda na wasaidizi
wake kuacha kutumia madaraka yao kuwanyima uhuru na haki wananchi na
kwamba Watanzania wanahitaji kuwaona wabunge wao wabovu na wazuri ili
mwaka 2015 wafanye maamuzi magumu ya kutokuwachagua au kuwachagua tena.
“Makinda
tumemwambia aache ubabaishaji katika uendeshaji wa Bunge. Watanzania
wanataka kuwaona wabunge wao wanaolala na wanaoshangilia hoja za hovyo!
Tunataka Bunge liendeshwe kwa mazingira yanayomwezesha mwananchi
kufahamu kila kitu kinachojadiliwa katika chombo hicho.
Akizungumzia
maamuzi ya CHADEMA kuanzisha uongozi wa kikanda, Mbowe ambaye pia ni
mbunge wa jimbo la Hai, alisema sera ya majimbo ni nguzo kubwa katika
kuleta maendeleo kwa wananchi, hivyo chama chake hakijakosea kufanya
hivyo na wanahitaji Tanzania igawanywe katika uongozi kwa ngazi ya
majimbo ili kurahisisha upatikanaji wa maendeleo.
Alisema
licha ya kwamba sera yao hiyo inabezwa na CCM, lakini ndiyo mkombozi
mkubwa katika adha ya umaskini miongoni mwa wananchi, hivyo wataisimamia
kikamilifu kuanzia sasa na baada ya kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu
ujao mwaka 2015.
Mbowe
aliishutumu CCM na viongozi wake kwa kueneza siasa mbaya za udini, kwani
walianza kuishambulia CUF kwa madai kwamba ni chama cha Kiislamu na
baadaye CHADEMA kwamba ni chama cha Wakristo, jambo ambalo kwa sasa
limejaa mbegu mbaya ya kuwepo kwa mzozo wa kidini na aliwataka
Watanzania kutokubali kugawanywa kwa ukabila, udini na ukanda na
wasiichague CCM 2015.
Mbali ya kauli ya Mbowe, matokeo hayo ya kidato cha nne yamelalamikiwa kila kona nchini.
Mwenyekiti
wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutangaza
tatizo la elimu kuwa janga la kitaifa na kumtimua Waziri Kawambwa.
Mbali na
Mbatia wadau mbalimbali na wananchi nao wametaka Rais Kikwete kuivunja
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuisuka upya.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mbatia alisema kuanguka kwa elimu
kumetokana na CCM kuendekeza mambo ya ushabiki wa kisiasa hata kwenye
mambo yanayolihusu taifa.
Mbatia
alieleza kuwa mitaala ndio dira ya elimu lakini akashangazwa na serikali
kutokuwa na mitaala rasmi na hata alipolieleza Bunge jambo hilo,
wabunge wa CCM walimjia juu na kuamua kuizima hoja hiyo.
“Serikali
haijawahi kuwa na mitaala rasmi, taifa halina dira ya elimu; kuna
mkanganyiko katika vitabu na ufisadi uliopo unaliangusha taifa hakuna
mfumo bali waziri anafanya anavyoamua,” alisema.
Alirejea
hoja yake kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kimejiaibisha kukataa hoja
yake na kueleza kuwa watoto wengi waliofeli ni wa CCM.
“CCM ndiyo
ina majimbo mengi kwa hiyo waliofeli ni watoto wao; sasa badala ya
kuhakikisha inaondoa kirusi katika elimu yenyewe inaingiza itikadi za
vyama katika suala la elimu.”
Aidha
alitaka vitabu vinavyotumika sasa mashuleni, vizuiwe na bajeti ijayo
vipengere kumi muhimu iwe ni elimu ili kunusuru anguko la sekta hiyo
kwani wizara iliyopo haiwezi kuyatatua peke yake.
Kwa upande
wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kauli ya
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, kuwa matokeo
hayo yameisikitisha serikali haitakuwa na maana yoyote kama haitakuwa na
jitihada za makusudi kuikwamua elimu ya Tanzania kutoka katika mfumo
uliopo sasa, Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafaunzo ya Ufundi,
Suzan Lyimo, alisema serikali imekuwa ikidharau kutatua matatizo ya
msingi inayoikabili sekta ya elimu.
Alitaja moja
ya matatizo ya walimu ni mazingira mabovu ya kufundishia, hali
inayowafanya wengi wao wasiwe na ari ya kufanya kazi hiyo.
“Serikali
imeisusa sekta ya elimu na hii ni kwa sababu viongozi wa serikali
hawawasomeshi watoto wao katika shule za serikali hivyo hawana uchungu
na matatizo yanayowakabili walimu na wanafunzi wa shule hizo,” alisema
Lyimo.
Aliongeza
kuwa hata katika masuala ya ukaguzi wa maendeleo ya elimu kama
ilivyokuwa zamani kwa sasa hautiliwi mkazo kutokana na bajeti finyu.
Naye Naibu
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri wa Elimu, Mafunzo
ya Ufundi, Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Phillipo Mulugo, kuwajibika
na kupisha katika wizara hiyo.
Pia alimtaka Rais Kikwete aichukue wizara hiyo na kuwa chini ya ofisi yake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa ni muhimu viongozi wanaosimamia wizara hiyo wakawajibika.
Alisema uwajibikaji huo unapaswa kufanyika kuanzia kwa katibu mkuu wa wizara hiyo pamoja na kamishna.
“Najua kuwa
haina uhusiano wa moja kwa moja maana matatizo ya elimu ni makubwa sana
nchini. Lakini ni lazima kitu fulani kitokee ili kufanya mabadiliko.
Uwajibikaji ni njia mojawapo inayoleta nidhamu na uharaka katika
utendaji kazi, alisema na kuongeza: “…namna hii (zaidi ya nusu ya
wahitimu kupata sifuri) na takriban asilimia 90 kufeli kwa kupata daraja
la nne na daraja la sifuri ni mwaka wa tatu sasa mfululizo. Matokeo
yakitoka tunasema weeee mpaka povu linatoka.
“Baada ya wiki tumeshasahau na hakuna hatua yoyote. Lazima uwajibikaji utokee,” alisema Zitto.
Alisema ni
muhimu Rais Kikwete aichukue Wizara ya Elimu, yaani Waziri wa Elimu awe
yeye, pia kuwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Elimu.
Zitto alisema kuwa Rais anapaswa aelezwe kuwa iwapo matokeo yatabaki hivi mwakani na yeye atatakiwa kuondoka katika nafasi hiyo.
“Najua wa
mwakani ndio wako kidato cha nne sasa na wana msingi mbaya tayari lakini
sio jukumu letu kujipa majibu bali ni jukumu letu kuiambia serikali;
hapana! Tuwape masharti. Vinginevyo haya yatakwisha na mwakani itakuja,”
alisema.
Zitto alisema elimu iliyopo sasa inazalisha matabaka ndani ya jamii na ni hatari kwa uhai wa taifa.
Mbali ya maoni hayo, wadau wengine walimtaka waziri mwenye dhamana ajiuzulu.
Mmoja wa wadau hao Selemani Juma, alisema kadri siku zinavyokwenda ndivyo anguko la elimu linavyozidi kuwa kubwa.
Alisema
mvurugano uliopo katika matumizi ya vitabu na kuacha vitabu vilivyokuwa
vinatumika na kuanza kutumia vitabu vingine ambavyo alidai vipo kwa
ajili ya maslahi ya viongozi, havina ubora na viwango vya kufundishia.
Naye Janeth
Alphonce, alieleza kuwa wizara husika chini ya Dk. Kawambwa, haiwezi
kutatua mifumo ya elimu ambayo ni ya miaka mingi na haiendani na soko la
elimu ya sasa.
Mwalimu John
Bosco Katatumba alisema matokeo hayo ni tafsiri ya hali ya ubovu wa
elimu nchini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Akitoa maoni
kwa njia ya simu, Lucas Nyangaramila (61), mkazi wa Arusha alisema
chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya ni mitaala ya elimu mibovu kwani
kila baada ya muda imekuwa ikibadilishwa.
“Mwanafunzi
aliyesoma kwa lugha ya Kiswahili kuanzia darasa la kwanza hadi la saba
na kusoma Kiingereza awapo sekondari ni vugumu kwake kuelewa lugha ya
Kiingereza mapema na badala yake kuongozwa na wale waliosoma shule za
Kiingereza kuanzia shule za msingi,” alisema.
Naye
Thobiace Boniface mkazi wa Mbezi Beach jijijini Dar es Salaam, alisema
matokeo ni mabaya na yanatia aibu na aliiomba serikali ifute shule za
kata kwa sababu ya maandalizi duni.
Hali
kadhalika, Mama Saidi mkazi wa Mabibo alisema kukua kwa sayansi na
teknolojia kumechangia kwa kiasi kikubwa kwa elimu ya wanafunzi kushuka
hapa nchini.
“Hii
mitandao kama vile intaneti, facebook, twitter n.k bila kusahau simu za
mikononi imekuwa ni kikwazo cha elimu kwa watoto wetu kwani wamekuwa
wakitumia muda mwingi kuwasiliana na watu mbalimbali kwenye mitando
hiyo, sasa muda wa kujisomea utatoka wapi?” alihoji.
Kwa upande
wake David Mlay, alisema kitendo cha shule za serikali kutofanya vizuri
hata kwa shule zake za vipaji maalumu ambazo ndizo zilikuwa tegemeo, ni
anguko kubwa la elimu nchini
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.