Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ameelezea kusikitishwa kwake na kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwamba chama hicho tawala kimekusanya maoni ya Katiba kwa Watanzania milioni mbili.
P.T
Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara wa kukusanya maoni ya Katiba, uliofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Turiani, Magomeni, Dar es Salaam Dk Slaa alisema: "Nimesikitishwa sana na kauli ya Kinana kwamba wamekusanya maoni ya Katiba yanayofikia milioni mbili jambo ambalo si kweli."
Alisema Chadema wamekuwa wawazi kwa kufanya mikutano yao nchi nzima, lakini hawakuwahi kusikia CCM wamekusanya maoni jambo ambalo alidai ni la ajabu kwa chama hicho kutaja idadi hiyo.
Akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Dodoma juzi, Kinana alisema CCM kimekusanya maoni milioni mbili ya wanachama kuhusu Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba, mchakato unaoendelea kupitia mabaraza.
Alidai kuwa Kinana alisema uongo kwa sababu hakuwahi kusikia maoni hayo yakikusanywa kama Chadema kinavyofanya kwa kuzunguka nchi nzima.
"Sisi tunafanya mikutano yetu ya kukusanya maoni ya Katiba kwa uwazi, lakini CCM wanatangaza kwa wanachama wao kwamba wamekusanya maoni milioni mbili bila kueleza njia wanazotumia... "Chadema imefanya mikutano ya kukusanya maoni nchi nzima na kufanya mikutano 48."
Katibu mkuu huyo wa Chadema pia alieleza kusikitishwa kwake na mapendekezo yanayotolewa na CCM kuhusu Katiba Mpya na kupingana na maoni ya Tume ya Katiba akisema kinapinga mambo mengi ya msingi.
"Kuna mambo ya msingi ambayo yana masilahi kwa taifa na wananchi kwa jumla, lakini wao (CCM), wanataka yasiwepo kwenye Katiba na wanapingana na Tume," alisema.
Baadhi ya mambo ambayo Dk Slaa aliyataja ni pamoja na ubaguzi, rushwa, dhuluma, vitisho na unyanyasaji ambayo alisema Rasimu ya Katiba imeyapa umuhimu kwa kuyatambua na kueleza kwamba hayapaswi kufanyika ili kulinda haki za wananchi.
"Ninasikitishwa na CCM kwamba kila jambo ambalo Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba ameona lina umuhimu kuwepo kwenye Katiba wao wanapingana nalo kitu ambacho ninaona hawana nia njema na maisha ya Watanzania na taifa kwa jumla," alisema.
Aidha, Dk Slaa alizungumzia tukio la kukamatwa kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe huko Iringa kwa madai ya kuvunja sheria kwa kuzidisha muda wa kufanya mikutano.
"Polisi ni watu wa kushangaza sana wamemkamata Mbowe kwa madai ya kuvunja sheria, ni kifungu gani kinachoeleza kwamba mtu anaweza kukamatwa kwa jambo hilo? Mimi naona kuna kitu wanachokitafuta kwa Chadema," alisema Dk Slaa.
Post a Comment