Mtuhumiwa katika kesi ya ugaidi, Abdallah
Maginga, ameiomba Mahakama ya Hakimu
Mkazi Arusha, kumruhusu kutohudhuria siku za
kesi na abaki magereza, kutokana na maumivu
makali anayodai anayapata sehemu za siri
alikominywa na polisi na kuingiziwa mti kwenye
haja kubwa.
“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako
inipe ruhusa ya kutohudhuria siku ya kesi,
sababu ninapopanda gari napata maumivu
makali sana sehemu za siri kunauma kwa
sababu polisi walinitesa kwa kuniingizia mti
kwenye haja kubwa na kuminya sehemu zangu
za siri,” alisema.
Alisema mbele ya Wakili wa Serikali, Rose Sulle
kuwa mbali na maumivu ya sehemu za siri, pia
mguu wake uliokatwa hospitalini, bado
unamsumbua kutokana na maumivu.
Maginga pia aliomba iagize Magereza
wamruhusu akatibiwe hospitalini, kwani
alitakiwa kwenda kupata matibabu Septemba 5
mwaka huu, ila alizuiwa hadi sasa.
Akijibu hoja hizo, Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo,
Devotha Msofe, alisema suala la kuja
mahakamani ni lazima na mahakama haiwezi
kumpa ruhusa hiyo.
Pia, alimshauri mshitakiwa huyo kuwa kama
ana maelezo mengi, amweleze hakimu
anayesikiliza kesi yake, Mustapher Siyani
ambaye kwa siku hiyo hakuwepo.
“Sikiliza Maginga suala la kuja mahakamani ni
lazima na sio hiyari wala majadiliano, ila
kuhusu kwenda hospitalini liwasilishe Magereza
ndio mtaona kwa pamoja mnafanyaje,” alisema.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa
washitakiwa hao wameshitakiwa kwa makosa
yaliyo chini ya Sheria ya Kuzuia ugaidi, ambapo
Sheria Namba 22 ya Mwaka 2002 inasema
upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo
yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya
kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha
vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Mbali na mashitaka hayo, pia wanahusishwa
na tukio la mlipuko wa bomu lilitokea baa ya
Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha
kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.
Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na
mashitaka hayo ni Abdallah Athumani, Abdallah
Thabiti, Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajab
Hemedi, Hassan Saidi, Ally Hamisi, Yassin
Sanga, Shaaban Wawa, Swaleh Hamisi, Abdallah
Yassin, Abdallah Maginga na Sudi Nassib
Lusuma.
Wengine walioongezwa katika shauri hilo ni
Shaaban Mussa, Athuman Hussein, Mohammed
Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohammed na Said
Michael Temba. Creadity mpekuzi
Post a Comment