Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku
maandamano ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), yaliyotarajiwa kuanza
kufanyika leo katika maeneo mbalimbali nchini.
Jeshi hilo limeonya kuwa maandamano hayo ni
batili na ni kinyume cha sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
makao makuu ya jeshi la Polisi Dar es Salaam,
Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo,
Paul Chagonja alisema jeshi hilo limeanza
kupokea taarifa ya chama hicho, kikitaka
kufanya maandamano kuanzia leo. Lakini,
alisisitiza kuwa maandamano hayo
hayataruhusiwa.
“Septemba 15 jeshi lilitoa taarifa kuhusu kauli
iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe akiwahimiza wafuasi wa
chama chake kufanya maandamano na migomo
isiyokoma pote nchini ili kusitishwa kwa Bunge
la Katiba na hivi sasa tumeanza kupokea taarifa
ya chama hicho kufanya maandamano,”
alisema.
Alisema maandamano hayo ni batili, kwa
sababu Bunge la Katiba linaloendelea hivi sasa,
linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba na hakuna sheria iliyokiukwa, hivyo
kitendo cha kufanya maandamano, kushinikiza
kuvunjwa kwa Bunge hilo ni kinyume cha
sheria, jambo ambalo jeshi la polisi haliwezi
kuruhusu.
Aidha, alisema kuwa ieleweke wazi kwamba
Bunge la Katiba, lipo kisheria na kila jambo
linalofanyika bungeni ni kwa mujibu wa sheria.
Chagonja alisema jeshi la polisi lina jukumu la
kulinda watu wote, wanaotekeleza majukumu
yao kwa mujibu wa sheria.
“Hata hivyo, hivi sasa kuna kesi inayoendelea
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
inayohoji uhalali wa kuendelea kwa Bunge hilo
na kesi hiyo haijafikia mwisho na uamuzi
kutolewa, hivyo maandamano hayo
yaliyopangwa na Chadema yanaingilia uhuru wa
Mahakama, jambo ambalo siyo sahihi.
Mahakama kama chombo cha kutoa haki,
kiachwe kifanye kazi yake,” alisema.
Chagonja alitoa mwito kwa wananchi wote,
kuendelea na shughuli zao na yeyote
atakayekiuka katazo hilo, jeshi la polisi halitasita
kumchukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Wakati Chagonja akiyasema hayo, Kamanda wa
Polisi mkoani Dodoma, amewaonya wafuasi wa
Chadema wanaodaiwa kutaka kuandamana
hadi Viwanja vya Bunge
kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la
Katiba.
Hata hivyo, uongozi wa Chadema mkoani
humo, umedaiwa kusisitiza maandamano yako
palepale.
Akizungumza jana, Kaimu Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula alisema
maandamano hayo, pia yamepangwa kufanyika
katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma.
Alisema juzi walipokea taarifa kutoka kwa
Uongozi wa Chadema Mkoa wa Dodoma, juu ya
kufanya maandamano ya amani kuanzia
viwanja vya Nyerere Square hadi viwanja vya
Bunge kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 6
mchana.
Alisema taarifa ya maandamano kama hayo,
yanayotarajia kufanyika katika wilaya zote za
mkoa wa Dodoma, ilitolewa jana ambapo ni
muda ulio kinyume na sheria ya kutoa taarifa
za maandamano ndani ya saa 48.
Alisema katika barua ya chama hicho kwenda
kwa Jeshi la Polisi, viongozi wa Chadema wa
Mkoa huo, walisema wanapinga Bunge la
Katiba na wanataka kupaza sauti zao, zisikike
dunia nzima na walisisitiza kufanya
maandamano hayo leo.
“Walikuja hapa viongozi wa Chadema Mkoa,
tulikaa nao kwenye mazungumzo zaidi ya saa
mbili, tuliwaambia Bunge lipo kwa mujibu wa
sheria za nchi na hakuna mahakama iliyotamka
Bunge lisitishwe, lakini walisisitiza kuwa
maandamano yako pale pale,” alisema.
“Maandamano hayo ni batili yanapinga chombo
ambacho kipo kwa mujibu wa sheria,
tunasisitiza wananchi wa Dodoma wasishiriki
maandamano hayo, hayana tija hata kidogo na
wananchi wasijitokeze waendelee na shughuli
zao,” alisema.
Alisema maandamano ni haki ya kikatiba, lakini
wanatakiwa kufuata sheria. Alisema Jeshi la
Polisi limejipanga kudhibiti maandamano hayo
katika wilaya zote, kutokana na viongozi wa
Chadema kukaidi amri ya kutaka kusitisha
maandamano hayo.
Wakati jeshi la Polisi likichukua hatua hiyo,
Umoja wa Vijana Wazalendo wa Vyuo vya Elimu
ya Juu Dar es Salaam, nao umejitokeza na
kulaani kauli zilizotolewa na Mbowe za
kuhamasisha maandamano na migomo nchi
nzima, hata kama jeshi la Polisi halitabariki
kufanyika kwa mambo hayo.
Mwenyekiti wa Umoja huo, Mussa Omar
anayesoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
(OUT), alisema umoja huo ni Muungano wa
vyuo 14 vya elimu ya juu vilivyopo Dar es
Salaam.
Alisema Watanzania wengi wamekerwa na
kusononeshwa na kauli ya kiongozi huyo ya
kuhamasisha maandamano, alizozitoa wakati
wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa
Chadema, mwishoni mwa wiki jijini Dar es
Salaam.
“Tumemsikia akiahidi maandamano bila kikomo
kwa kibali cha polisi au bila kibali cha polisi
mbele ya wajumbe na wageni ambao wengine
sio Watanzania,” alisema Omar.
Aliongeza kuwa kauli kama hiyo, haiwezi
kusemwa hata na Rais ambaye ni Amiri Jeshi
Mkuu.
Alimtaka Mbowe afahamu dhamana kubwa ya
uongozi aliyonayo kwa wafuasi wake na
Watanzania kwa ujumla, wakimtaka afuate
misingi ya sheria za nchi, katiba na utawala
bora.
Pia, alisema kauli zilizotolewa na Mbowe,
hazibebeki na mtu yeyote katika taifa hili,
kwani alitoa kauli mbaya kuliko zote kisiasa,
ambazo zimewahi kusemwa majukwaani.
“Watanzania tukikaa bila kuzilaani na
kuzikemea kauli zake tutakuwa hatujitendei
haki sisi wenyewe na pia hatuvitendei haki
vizazi vijzvyo vya nchi yetu,” aliongeza.
Alihoji uhalali wa kutoa amri hizo kwa wafuasi
wake, ilhali ni kiongozi tu wa chama, tena
ambacho hakiko madarakani.
Alisema Watanzania wanapaswa kuwakataa
viongozi wenye jazba na kutumia mabavu katika
kutimiza majukumu yao, kwani wanaweza
kuiingiza nchi katika vurugu zisizo na ulazima.
Pia alivitaka vyombo vya dola, visizivumilie kauli
kama hizo, zilizotolewa na Mbowe, kwani
vyombo vya dola vina dhamana ya kulinda,
kutunza na kuendeleza amani na utulivu wa
nchini, wachukue hatua kali za kisheria kwa
kauli ya kutishia uvunjifu wa amani kabla
hajaingiza nchi kwenye machafuko ya kisiasa.
Wakati huo huo, viongozi wa juu wa chama
hicho, leo wamepanga kumsindikiza Mbowe
kwenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini,
ambako ameitwa kwa barua.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa
alisema Mbowe alipokea barua, ikimtaka afike
Makako Makuu ya jeshi hilo leo saa 5:00
asubuhi.
“Mwenyekiti wetu ameitwa Makao Makuu ya
Polisi leo na hatujui kaitiwa nini, huenda
anakwenda kuhojiwa na huenda mwito huo
umetokana na kauli alizotoa awali katika
mkutano mkuu, ambazo zililenga kuhamasisha
maandamano ya nchi nzima kupinga Bunge la
Katiba linaloendelea”, alisema Dk Slaa.
Alitaja watakaoongoza msafara wa amani wa
kumsindikiza Mbowe kuwa ni mwanasheria
wao, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara),
Profesa Abdallah Safari na Mwanasheria Peter
Kibatala.
Hata hivyo, alisema pamoja na kiongozi huyo
kuitwa na polisi, bado jeshi hilo haliwezi
kuvunja ajenda ya kuandamana, kwa kuwa
ilipitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho, na
kwamba polisi wao wanapaswa kutoa kibali cha
kuruhusu maandamano hayo.
Awali, alisema maazimio yaliyopitishwa na
Kamati Kuu ya chama hicho ni kuunganisha
nguvu ya pamoja na vyama vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) .
Alisema maazimio hayo, yataanza Desemba 14,
mwaka huu, siku ambayo uchaguzi wa serikali
za mitaa unaanza.
Alieleza kwamba chama hicho kimeunda kamati
ya watu watano, itakayoangalia jinsi ushirikiano
wa Ukawa utakavyokuwa kwenye uchaguzi huo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kutoka kwao nje
bungeni, kulikuwa sahihi. Alisema katiba mpya,
haiwezi kupatikana leo au kesho
Post a Comment