Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba watishiwa maisha.....Vipeperushi vyasambazwa kila kona ya mkoa wa Dodoma

Siku tatu kabla ya Bunge la Katiba kuanza
kupigia kura Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa, watu wasiojulikana
wameanza kusambaza vitisho vya kuwatia hofu
wajumbe wa Bunge hilo.
Watu hao wamesambaza vipeperushi katika
maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma usiku
wa kuamkia jana, wakiwataka wajumbe
kutoingia bungeni vinginevyo yatakayowapata
watajuta, huku wajumbe kutoka Zanzibar
wakitishiwa kwa ujumbe wa simu kupitia
mtandao wa WhatsApp.
Tayari, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Ali Idd ametoa kauli kuhusu vitisho
hivyo akisema Serikali itachukua kila hatua
kuhakikisha wajumbe kutoka visiwani humo
ambao wamekuwa wakipokea vitisho wanakuwa
salama.
Mbali na kusambazwa kwa karatasi hizo,
maandishi mekundu yamechorwa katika kuta za
jengo la Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma
yakisomeka, “No Katiba. No ufisadi.”
Vikaratasi vilivyosambazwa vinasomeka: “Onyo.
Dodoma si mahali pa kufuga wezi wa fedha za
umma. Utakayeingia bungeni kuanzia kesho
(leo), yatakayokupata utajuta.”
Mkazi wa Dodoma, Sospeter Samwel
alimwambia mwandishi wetu jana kuwa
aliokota baadhi ya vipeperushi hivyo jana saa
moja asubuhi katika eneo maarufu la kuuzia
magazeti linalotazamana na Jengo la CCM.
“Tulikuta hayo makaratasi yametupwa tu
ovyoovyo ila baadaye nikasikia maeneo
mbalimbali mengine nayo yameonekana
yametupwa. Sijui nani hasa watakuwa
wameyasambaza,” alisema.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alipoulizwa jana kuhusu na maandishi
hayo alijibu kwa kifupi “No comment” (sina cha
kusema).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David
Misime jana alitoa taarifa ya maandishi kwa
wanahabari akisema jeshi hilo linawasaka watu
waliosambaza vipeperushi hivyo.
“Wananchi na wageni wapenda amani
waendelee na shughuli zao kama kawaida
kwani polisi tumejiimarisha ipasavyo
kukabiliana na yeyote atakayekiuka sheria na
maelekezo yaliyotolewa."
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema
Nchimbi alitoa onyo kwa watu aliodai
wanafanya mzaha akisema vyombo vya
usalama viko macho saa 24. Aliwataka
wajumbe kutoa taarifa kwa vyombo vya dola
wanapoona viashiria vya kutokuwa na usalama.
“Kama ng’ombe mzima tumeshakula
tumebakiza mkia tu, niwahakikishie wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba, usalama
umekuwapo na utaendelea kuwapo."
Wazanzibari kulindwa
Akizungumzia vitisho hivyo hasa kwa wajumbe
kutoka Zanzibar, Balozi Idd alisema Serikali
itachukua kila hatua kuhakikisha wanakuwa
salama.
Alisema kuna ujumbe unazunguka katika
mitandao ya jamii ukitoa vitisho kwa wajumbe
wa Bunge hilo na watumishi wa sekretarieti ya
Bunge hilo.
“Vyombo vya dola vipo na vitafanya kazi yake.
Vinajua vitisho vyote. Niwahakikishie wajumbe
mtakuwa salama na Serikali itachukua kila
hatua kuhakikisha hakuna kitakachotokea."
Hoja 17 za Zanzibar
Akizungumzia kuhusiana hoja 17 ambazo
ziliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Othman Masoud Othman zenye
masilahi ya visiwa hivyo, Balozi Idd alisema kati
yake 13 zilikubalika na kubakia nne.
Hata hivyo, alisema baada ya kuangalia zaidi
Rasimu ya Katiba inayopendekezwa waligundua
kuwa zilibakia hoja tatu tu.
Alizitaja hoja hizo kuwa ni ibara 86 ambayo
inasema Rais wa Jamhuri ya Muungano
atashinda kwa kupata kura zaidi ya asilimia 50.
Hata hivyo, alisema waliona kwenye Katiba ya
sasa jambo hilo liko kimya kidogo endapo
itatokea mgombea hakupata kura upande wa
Zanzibar.
“Tukaona kuwa huyu ni Rais wa Muungano, hivi
asilimia 50 yote apate Bara legitimacy (uhalali)
yake kama rais wa Muungano iko wapi?”
alisema na kuongeza kuwa vyema katika
Rasimu ikaingizwa kuwa mgombea huyo pamoja
na kwamba anatakiwa ashinde kwa zaidi ya
asilimia 50, basi angalau katiba iweke kiwango
fulani cha kupata upande wa Zanzibar.
Alisema baada ya kutafakari ikakubaliwa
Zanzibar angalau mgombea huyo apate asilimia
10 au 15. Hata hivyo, alisema majadiliano
kuhusu suala hilo bado yanaendelea.

Post a Comment

Contact Form

Name

Email *

Message *

designed by izack. Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget