Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha)
limetangaza maandamano kwenda Ikulu
kumuomba Rais Jakaya Kikwete asikubali kutia
saini Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iwapo
itapitishwa na Bunge.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee alisema
jana kwamba maandamano hayo yatafanyika
mwishoni mwa wiki ijayo, baada ya maandalizi
yatakayofanyika kwa siku saba kuanzia jana
kukamilika.
Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe, alisema
baraza hilo limeamua kuitisha maandamano
hayo ili kuwakilisha kilio cha wanawake ambao
ndiyo waathirika wa kwanza pale nchi
inapokuwa katika mfumo usio wa haki.
Alivitaka vyombo vya dola hasa polisi kujitokeza
kuwasindikiza na kuandamana nao kwa kuwa
nao ni miongoni mwa Watanzania ambao
wataathiriwa na uamuzi usiolenga kujenga
umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, Polisi imetahadharisha kuwa
itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria
wanachama wa Chadema watakaojiingiza katika
maandamano yaliyopigwa marufuku nchini.
Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alisema,
“Kauli yetu haijabadilika, maandamano ya
Chadema ni batili. Yeyote atakayeandamana
atakuwa anakiuka utii wa sheria bila shuruti.
“Jukumu letu ni kuwalazimisha wote wasiotaka
kufanya hivyo, kuitii kwa shuruti.”
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa
Salum amewataka Watanzania kutokuwa na
papara ya kupata Katiba Mpya kwani mwisho
wa siku wenye uamuzi wa kutaka iwe ya
namna gani ni wao.
“Ni vyema na busara Watanzania wakasubiri
na kuliachia kazi Bunge hilo Maalumu ambalo
linamaliza kazi hivi karibuni na wao kubaki na
kazi ya kuchagua wanachokitaka kiwemo
kwenye katiba hiyo."
Maandamano yazimwa
Polisi wamedhibiti wafuasi wa Chadema
maeneo mbalimbali waliokuwa wamejipanga
kufanya maandamano na wengine
wamefikishwa kortini.
Wanachama zaidi ya 40 wa Chadema eneo la
Mbalizi, Mbeya Vijijini walikumbana na virungu
vya polisi muda mfupi baada ya kuanza
maandamano katika Mtaa wa Z.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya, Ahmed Msangi alisema hakuwa na
taarifa yoyote lakini angependa wakazi wa
Mbeya wafikirie zaidi masuala ya elimu,
biashara na kilimo kuliko siasa.
Katavi
Viongozi watatu na wafuasi 14 wa Chadema
Mkoa wa Katavi wanashikiliwa na polisi kwa
tuhuma za kufanya maandamano bila kibali.
Wanachama hao walikamatwa jana saa nne
asubuhi eneo la Zahanati ya Kasimba katika
Mtaa wa Majengo A, wakiwa wanaandamana
kwenda Viwanja vya Hoteli ya Mpanda
walikopanga kufanya mkutano.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri
Kidavashari alisema wanaoshikiliwa ni: Katibu
wa Chadema wa Mkoa, Almasi Ntije,
Mwenyekiti Wilaya ya Mpanda, Abraham
Mapunda na Katibu wa Jimbo la Mpanda Mjini,
Cretus Nkumba.
13 wanaswa Mwanza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino
Mlowola amesema wanawashikilia watu sita
baada ya kukutwa wamejikusanya katika
makundi jambo lilioashiria walitaka
kuandamana.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Mwanza, Adrian Tizeba alisema wanaoshikiliwa
ni wanachama 13 na viongozi wao. Aliwataja
baadhi ya viongozi wanaoshikiliwa kuwa ni
Mwenyekiti wa Chadema Vijana Mkoa, Joseph
Idd, Mwenyekiti Wilaya ya Nyamagana,
Josephat Nungwana na Katibu wa Vijana Wilaya
ya Ilemela ambaye hakumtaja.
Dar es Salaam
Wafuasi 12 Chadema wamefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na mashtaka ya kufanya
mkusanyiko usio halali kwa nia ya
kuandamana.
Wakili wa Serikali, Bernard Kongola aliwataja
washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi, Frank
Moshi kuwa ni Paulo Stanley ‘Ndege’, Joseph
Michael, Ajenta Emmanuel na Waziri Saidy
‘Mahunzi’.
Wengine ni Oldgard Lerio, Sifa Majura, Magreth
Mapunda, Remina Peter, Stella Masanja,
Mwanahamisi Hassani, Vaileth Seka na Sina
Manzi.
Kongola alidai mahakamani kuwa juzi katika
maeneo ya Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Ilala Boma walifanya mkusanyiko usio
halali kwa nia ya kuandamana kinyume cha
sheria.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili,
washtakiwa wote walikana na upande wa
mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo
umekamilika.
Washtakiwa hao walirudishwa rumande baada
ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana
na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 8
Post a Comment