WAKATI ikiwa imezoeleka kuwa baadhi ya
walimu wa kiume huwarubuni wanafunzi wao
wa kike na hata kuwaharibia kabisa ndoto zao
za kielimu kutokana na kuwapa ujauzito, hali
imekuwa tofauti mkoani Rukwa ambako
mwanafunzi wa Kidato cha Pili anadaiwa
kumzalisha mwalimu wake.
Mwanafunzi huyo aliyemzalisha mwalimu wake
ana umri wa miaka 17, wakati mwalimu huyo
anayefundisha katika Shule ya Sekondari ya
Umma ya Nkasi, iliyopo mwambao mwa Ziwa
Tanganyika wilayani Nkasi, Rukwa, ana umri wa
miaka 25.
Tukio hilo linalotajwa kuwa la kwanza kutokea
wilayani hapa, limekuwa gumzo kubwa kwa
wakazi wa Nkasi na wilaya jirani.
Hata hivyo, kwa wanafunzi, wamekuwa
wakimpongeza mwenzao kwa kujaliwa kupata
mtoto katika umri wake huo mdogo, huku mzazi
mwenzake akiwa na uhakika wa maisha
kutokana na kuwa ni mtumishi serikalini.
Imeelezwa kuwa licha ya tukio hilo, mwalimu
huyo aliyezaa na mwanafunzi wake bado
anaendelea na masomo shuleni hapo, huku
`mzazi’ huyo wa kiume akifundishwa na mzazi
mwenzake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini
Namanyere hivi karibuni, Mkuu wa Shule ya
Sekondari Nkasi mjini Namanyere ambayo ni ya
mchanganyiko ya umma, Amiamie Nanga
alisema mwalimu huyo alianza kazi shuleni
hapo ikiwa ni mara yake ya kwanza kufundisha
baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu chuoni.
“Yameshatokea, lakini haileti picha nzuri sana,
lakini mimi nina uzoefu mkubwa na wakazi wa
mwambao wa Ziwa Tanganyika, kwao si ajabu
kuwa na uhusiano na watu waliowazidi umri,
iwe kwa mtoto wa kike au wa kiume, wote ni
sawa tu…
“Lakini katika kisa hiki, inaonesha walimu sasa
wanapoteza haiba ya ualimu. Hii kazi ina miiko
na maadili yake …kwa mwalimu huyu hii ni
ajira yake ya kwanza, nikimaanisha ni kituo
chake cha kwanza cha kazi tangu ahitimu
masomo yake…” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema
hakuna kosa kwa mwalimu huyo wa kike kwa
kuwa tayari ni mtu mzima.
“Isitoshe katika kisa hiki ni nadra kumpata
mlalamikaji … Mwalimu mwenyewe huyu wa
kike hawezi kuwa tayari kujidhalilisha kuwa
amebakwa, yalikuwa maamuzi yake.”
Aliongeza kuwa, kwa mwalimu huyo kupata
ujauzito wa mwanafunzi wake hakuwezi kuathiri
ajira yake, tofauti na mwalimu wa kiume
akimpatia ujauzito mwanafunzi wake wa kike
ambaye huathirika kwa kukatisha masomo.
Jitihada za kumpata mwalimu huyo wa kike na
mwanafunzi huyo zimegonga mwamba baada
ya watu wao wa karibu kumweleza mwandishi
kuwa hawako tayari kuuzungumzia mkasa huo.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo waliohojiwa
na mwandishi wa habari hizi kwa masharti ya
kutoandikwa majina yao kwa hofu ya
kuchukuliwa hatua za kinidhamu shuleni hapo,
pamoja na kukiri kutambua uhusiano baina ya
mwanafunzi mwenzao na mwalimu wao, lakini
walisema hivi sasa mwalimu huyo amesitisha
uhusiano na mwenzao na kuanzisha uhusiano
mpya na mwalimu mwenzao.
Walisema pamoja na mambo mengine ni kama
mwanafunzi mwenzao ameathirika kisaikolojia
baada ya ‘kupinduliwa’ na mwalimu wake wa
kiume ambaye kwa sasa ndiye baba mlezi wa
mtoto.
“Huyu mwalimu wa kike sisi sasa tunamwita
shemeji yetu alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na mwenzetu… penzi lao lilikolea
hadi sasa ameweza kumzalia mtoto huyo…,
lakini kwa sasa inavyoelezwa ni kwamba penzi
limehamia kwa mwalimu mwenzake,“ alisema
mmoja wao.
Baadhi ya watu wa karibu na mwanafunzi huyo
wanakiri kuwa mwanafunzi huyo hana uwezo
wa kifedha kumudu kumpatia malezi stahiki
mtoto wake huyo, hivyo hata mzazi mwenzake
alipoanza uhusiano na mwalimu mwenzake
hakuwa na jinsi, bali kukubaliana na matokeo.
“Usiniandike jina, sisi tunashauri mwalimu huyo
wa kike na mpenzi wake huyo wa kiume
ambaye ni mwalimu mwenzake wahamishiwe
shule nyingine kwa sababu kama kioo katika
jamii wameteleza kwa kiasi kikubwa na
watashindwa kuwajenga na kuwalea wanafunzi
wao kimaadili.
“Isitoshe tunajiuliza sheria hapa inasemaje
maana kama angekuwa ni mwalimu wa kiume
amempatia mwanafunzi wake wa kike ujauzito
angeshitakiwa na kufikishwa mahakamani na
pengine kuhukumiwa kifungo kisichopungua
miaka 30 jela, sasa kwa hili sheria inasemaje?”
Alihoji.
Baadhi ya wazazi mkoani hapa waliohojiwa na
mwandishi kwa nyakati tofauti wameelezea
kushangazwa na tukio hilo, na hasa kwa jinsi
mwalimu alivyoshindwa kujizuia `kujiachia’
kimapenzi kwa mwanafunzi wake.
Credit: Habarileo
Post a Comment