Rais Kikwete Avunja Rekodi ya Dunia ....Apokelewa kwa pikipiki za Polisi China na kuongozwa na pikipiki hizo kwa muda wote wa ziara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesababisha mageuzi makubwa kwa namna
Jamhuri ya Watu wa China inavyowapokea
viongozi wageni kutoka nje kwa kuwa kiongozi
wa kwanza duniani kupokewa rasmi na pikipiki
za polisi na kuongozwa na pikipiki hizo kwa
muda wote wa ziara katika kipindi cha miaka
10 iliyopita.
Rais Kikwete ambaye aliwasili nchini China
Jumanne iliyopita, Oktoba 21, 2014, kuanza
ziara rasmi ya siku sita nchini humo, amekuwa
kiongozi wa kwanza wa nje kupokelewa na
msafara wa pikipiki tokea Januari Mosi, mwaka
2004, miaka 10 iliyopita wakati China ilipofuta
utaratibu wa misafara ya viongozi kusindikizwa
na pikipiki za polisi.
Rais Kikwete na msafara wake alipokewa na
msafara wa pikipiki wa polisi mara baada ya
kuwasili Uwanja wa Ndege wa Beijing hadi
kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali
ya Diaoyutai, katikati ya Jiji la Beijing na
utaratibu huo kuendelea kuongoza msafara
wake kwa siku zote alipokuwa China.
Taarifa ya habari iliyotolewa na Wizara ya
Mambo ya Nje ya China na kukaririwa na
Shirika la Habari la nchi hiyo la Xinhua haikutoa
sababu zozote za mabadiliko ya sera hiyo.
Katika nchi karibu zote duniani, utaratibu wa
viongozi wa nchi mbali mbali kupokelewa kwa
misafara ya pikipiki ni protokali ya juu kabisa
ambayo pia huongeza usalama wa kiongozi na
ni utaratibu wa kawaida katika nchi nyingi
duniani.
Tokea kuasisiwa kwake mwaka 1949, Jamhuri
ya Watu wa China ilikuwa na utaratibu wa
pikipiki za polisi kuongoza misafara ya viongozi
lakini utaratibu huo ulisimamishwa Januari
Mosi, mwaka 2004, kwa sababu ambazo
hazijapata kuelezwa.
Baada ya kuweka historia hiyo ya kuwa kiongozi
wa kwanza wa nchi ya kigeni kupokelewa na
msafara wake kuongozwa na msururu wa
pikipiki nane, Rais Kikwete anatarajiwa
kuondoka China leo, Jumatatu, Oktoba 27,
2014, baada ya kuwa amemaliza ziara yake
rasmi.
Rais Kikwete anatarajiwa kuanza ziara rasmi ya
siku mbili katika Vietnam kwa mwaliko wa
Mheshimiwa Truong Tan Sang, Rais wa Jamhuri
ya Kisoshalisti ya Vietnam ambako miogoni
mwa mambo mengine nchi hizo mbili
zitaadhmisha miaka 50 tokea kuanzishwa kwa
uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili.
Miongoni mwa shughuli zake kubwa, Rais
Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na
Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha
Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Phu Trong na
Mwenyekiti wa Bunge la Vietnam, Mheshimiwa
Nguyen Sinh Hung.
Aidha, Mheshimiwa Rais atatembelea taasisi
mbalimbali zenye uhusiano wa kiuchumi na
Tanzania ikiwemo Kampuni ya Viettel inayotaka
kuwekeza katika mawasiliano ya simu za
maeneo ya vijijini katika Tanzania kwa bei
nafuu zaidi.
Share 1

Post a Comment

Contact Form

Name

Email *

Message *

designed by izack. Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget