Serikali ya Nigeria imesema wamefikia makubaliano ya kusitisha
mapambano na kikundi cha wapiganaji wa Boko Haram, ambapo katika taarifa
rasmi iliyotolewa kuhusiana na makubaliano hayo imesema kuwa
wameafikiana kuhusu kuachiliwa huru kwa wasichana zaidi ya 200
waliotekwa nyara huko Chibok.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa serikali ya Nigeria, Hassan Tukur
amesema maafikiano hayo yamefikiwa leo baada ya kumalizika kwa
mazungumzo baina ya upande wa serikali na wawakilishi wa kikundi hicho,
yaliyodumu kwa takribani mwezi mmoja.
Serikali imesema imekuwa ikifanya mazungumzo na viongozi wa Boko
Haram mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na yale yaliyofanywa mara mbili
nchini Chad chini ya uongozi wa Rais wa Chad, Idris Derby.
Tukur amesema kuwa Boko Haram wamekubali kuwaachilia huru wasichana
waliotekwa nyara mjini Chibok, japo muafaka zaidi juu ya hilo
utapatikana punde baada ya kumalizika mkutano mwingine unaotarajiwa
kufanyika wiki ijayo nchini Chad.
Bado haijafahamika kama makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande hizo
mbili yanahusisha na matakwa yaliyotolewa awali na kundi la Boko Haram
kutaka kubadilishana wasichana hao na wafungwa ambao ni wapiganaji wa
kikundi hicho wanaoshikiliwa na serikali ya Nigeria.
Post a Comment