Serikali Tanzania ichunguze kashfa ya pembe za ndovu
Serikali ya Tanzania imetakiwa ifanye uchunguzi wa kimataifa kubaini
watu waliohusika na ripoti iliyoitia doa serikali kuhusu madai ya
kusafirishwa pembe za ndovu kwenye ndege ya Rais wa China, Xi Jinping.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni na Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph
Mbilinyi wakati akichangia mapendekezo ya utekelezaji wa mpango wa taifa
kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Mbunge huyo wa chama kikuu cha upinzani
cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA amesema kuwa, serikali isije na
kauli nyepesi kama ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, kuwa taarifa hizo ni za uzushi na badala yake
ifanye uchunguzi. Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano maalumu na
idhaa hii ya Radio Tehran, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba Mwenyekiti
Taifa wa Chama cha Upinzani cha Wananchi CUF alielezea kusikitishwa
kwake na mitandao ya ufisadi na ujangili iliyokita mizizi serikali na
kubainishwa kwamba, umefika wakati sasa kwa Watanzania kuleta mabadiliko
ya uongozi ili kuokoa utajiri na rasilimali za nchi zinazoporwa huku
serikali ya chama tawala CCM ikionekana kushindwa kukabiliana na wimbi
hilo la uporaji.
Post a Comment