MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewaachia huru wafanyabiashara watatu,
wakiwemo mume na mke, waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 13 na
miezi sita jela kwa sababu ya wizi wa Sh bilioni 1.1 katika Akaunti ya
Madeni ya Nje ya (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Walioachiwa huru ni mume Manase Makale na mkewe Edda Makale, na mfanyabiashara mwingine Bahati Mahenge.
Washitakiwa hao waliachiwa mwisho wa wiki iliyopita baada ya Jaji
Augustine Shangwa kukubali rufaa iliyowasilishwa na wafanyabiashara hao
kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka
jana.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Shangwa alisema anawaachia huru
wafanyabiashara hao kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kabisa
kuthibitisha mashitaka dhidi yao.
Aliamuru wafanyabiashara hao waachiwe huru mara moja na kutengua amri ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyowataka warejeshe fedha hizo mara
baada ya kutumikia kifungo.
Katika rufaa, wafanyabiashara walikuwa wakipinga hukumu iliyotolewa na
jopo la mahakimu Sekela Mushi, Sam Rumanyika na Lameck Mlacha, wakidai
kuwa kulikuwepo na upungufu mkubwa wa kisheria na kihoja katika kuwatia
hatiani.
Katika hukumu iliyotolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahenge
alitakiwa kutumikia kifungo cha miaka saba jela, Makale kifungo cha
miaka mitano jela na mkewe Edda kifungo cha mwaka mmoja na nusu.
Aidha, mahakama iliamuru baada ya kutumikia adhabu hiyo, Mahenge na
Makale warejeshe kiasi cha Sh bilioni 1.18 walichodaiwa kukiiba katika
akaunti ya EPA.
Washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kutenda
kosa, kughushi nyaraka mbalimbali na kuziwasilisha sehemu husika na
kuiba fedha hizo.
Katika kesi hiyo, wafanyabiashara hao walikuwa wameshitakiwa na wenzao
Davis Kamungu na Godfrey Mushi ambao waliachiwa huru katika Mahakama ya
Kisutu kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka
dhidi yao bila kuacha shaka.
Chanzo: Habari Leo
Post a Comment