BIBI WA MIAKA 90 ASIMULIA ALIVYOLAWITIWA USIKU KUCHA...
BIBI WA MIAKA 90 ASIMULIA ALIVYOLAWITIWA USIKU KUCHA...
Ajuza wa miaka 90, amedai mahakamani jinsi alivyolawitiwa usiku kucha na kijana wa rika la mjukuu wake baada ya kuvunja mlango na kuingia ndani.
Kabla ya kutoa ushahidi huo, hivi karibuni Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, ililazimika kuhamisha kesi kutoka Mpanda Mjini hadi ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Bulembo, anakoishi bibi huyo.
Bibi huyo (jina limehifadhiwa), alitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Mpanda, Chiganga Tengwe, akiwa amekaa kwenye mkeka, kutokana na umri mkubwa lakini pia matatizo ya kupooza viungo.
Akiwa shahidi wa tatu kati ya wanne waliotoa ushahidi wao, bibi huyo alidai kwamba usiku wa Desemba 22 mwaka jana, mshitakiwa Sindebula Msangi (32), alivunja nyumba yake na kumwingilia kwa nguvu kinyume cha maumbile.
“Bahati mbaya sana mimi naishi pekee yangu, hivyo usiku huo mshitakiwa alivunja mlango wa nyumba yangu, akanishika kwa nguvu. Nilimsihi hivi unanifanyia hivi, mbona kuna mabinti wengi mtaani?
“Lakini alikaidi na kutimiza azma yake akaniingilia kinyume cha maumbile na kunijeruhi na kunisababishia maumivu makali,“ alidai.
Alidai kuwa usiku huo, mshitakiwa aliendelea kumlawiti mara kadhaa, mpaka alipochoka na kusinzia chumbani humo baada ya kupitiwa na usingizi mzito.
Kwa mujibu wa bibi huyo, ilipofika saa 12 asubuhi, mshitakiwa akiwa amelala fofofo, alifungua dirisha la chumba na kumwita mpitanjia aliyemtambua kwa jina la Ashabola Elly.
Alidai alimwita Ashabola kwa ishara ya vidole akaja na kuingia chumbani ambamo alimkuta mshitakiwa amelala fofofo.
Bibi huyo alidai kuwa Ashabola alinyata na kutoka nje ya nyumba hiyo, bila kumwamsha mshitakiwa huyo na kutoa taarifa kwa majirani na uongozi wa kijiji hicho.
Hata hivyo, kwa mujibu wa bibi huyo, majirani na viongozi hao walipofika nyumbani hapo mshitakiwa alikuwa tayari ameamka na kutokomea kusikojulikana kwa muda, hadi alipokamatwa baadaye.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 22 mwaka jana saa nane usiku kijijini Bulembo, katika kambi ya wakimbizi ya Katumba.
Mshitakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 28 mwaka jana.
Hata hivyo alikana mashitaka na Hakimu Tengwe aliamuru mshitakiwa arudishwe rumande hadi Machi 28, atakapojitetea.
Post a Comment