KATIBU Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
amesema wamenasa nyaraka na
viashiria mbalimbali
vinavyoonyesha kuwa Chama Cha
Mapinduzi kinakusudia kuharibu
mchakato wa katiba.
Dk. Slaa, alitoa kauli hiyo juzi
usiku jijini Mwanza katika kipindi
cha ‘Ajenda 2015’, kinachorushwa
moja kwa moja na kituo cha
televisheni cha Star Tv.
Kiongozi huyo alikuwa akijibu
swali la mtangazaji wa kipindi
hicho, Dotto Bulendu, aliyetaka
kujua ni kwanini Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA) wameamua
kuanza ziara mikoani
kuwaelimisha wananchi wakati
mchakato wa katiba ndio upo
katika hatua ya rasimu ya pili
kujadiliwa bungeni.
Akijibu swali hilo, Dk. Slaa,
alisema wananchi
wamechanganywa kwa kuwa
waliambiwa wakusanye maoni yao
na kuyapeleka katika Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa
chini ya Jaji Joseph Warioba,
lakini Rais Jakaya Kikwete
kaidharau.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Jakaya Kikwete
alipoenda kuzindua Bunge,
alitumia muda huo kutoa semina
elekezi na kutangaza msimamo wa
Chama Cha Mapinduzi ambao
haukujali maoni ya wananchi,”
alisema Dk. Slaa.
Alisema Watanzania wanapaswa
kuelewa kuwa CHADEMA
walipokuwa wanapigania sheria ya
mabadiliko ya katiba kutaka rais
asiwe na mamlaka makubwa katika
kuteua wajumbe wa Bunge
Maalumu, walibaini athari za
mchakato kutekwa na chama
tawala.
Alibainisha kuwa msemaji wa
kambi rasmi ya upinzani kuhusu
mambo ya katiba na sheria, Tundu
Lissu, aliyekuwa akipinga jambo
hilo, alionekana ni mbishi,
asiyependa kuwasikiliza wengine,
lakini athari ya uteuzi inaonekana
sasa.
Dk. Slaa, alisema wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba asilimia
kubwa ni wanachama wa CCM kwa
kivuli cha kupitia kwenye asasi
mbalimbali.
Alisema vyama vinavyounda
Ukawa, vimeamua kwenda kwa
wananchi nchi nzima kuwaeleza
ukiukwaji wa kanuni uliofanywa
kwa makusudi na Mwenyekiti wa
Bunge la Katiba, Samuel Sitta,
ambaye aliruhusu Jaji Warioba
awasilishe rasimu kabla ya hotuba
ya ufunguzi ya Rais Kikwete.
Alibainisha kuwa kilichofanywa na
Sitta kililenga kutoa fursa kwa
Rais Kikwete kuwachanganya
wananchi kwa kupinga maoni ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
aliyoiunda.
Dk. Slaa, aliongeza kuwa Ukawa
wamejitokeza sasa kutokana na
serikali kutumia nguvu nyingi
ikiwemo vyombo vya habari
kuchakachua maoni ya wananchi.
“Tume ni ya rais mwenyewe,
ilitumwa kukusanya maoni na yeye
mwenyewe, hadidu za rejea alitoa
yeye, na ushahidi upo amefanya
mahojiano ya mara kwa mara na
tume, hivyo kuja kukataa maoni ya
wananchi, ni dharau na matusi
kwa Watanzania waliotoa maoni,”
aliongeza Dk. Slaa.
Dk. Slaa, alikemea matamko
yanayotolewa na baadhi ya watu
kukataa kuheshimu maoni ya
wananchi, akitolea mfano kauli ya
Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana aliyoitoa wiki
iliyopita katika viwanja vya
Mwembeyanga, Temeke jijini Dar
es Salaam.
Akihutubia mkutano wa
wanachama wa CCM, Kinana
alikaririwa akisema; “mchakato wa
katiba mpya unaoendelea bungeni
mjini Dodoma, msimamo wa CCM
utaendelea kuwa ni serikali mbili.”
Alisema hotuba iliyotolewa na Rais
Kikwete, wakati akizindua Bunge
la Katiba, imetoa mwelekeo mpya
kwa wajumbe wa Bunge.
Mchangiaji mwingine katika
kipindi hicho aliyejulikana kama
Solomon Lufunda aliyekuwa katika
kipindi hicho upande wa Dar es
Salaam, alisema kuwa mchakato
wa katiba umeingiliwa zaidi na
serikali na kuwanyima wananchi
fursa.
Lufunda alisema kuwa CCM
imeingilia na inavuruga mchakato
wa katiba, haiheshimu matakwa ya
wananachi.
Alikemea vikali kauli ya hofu
iliyosemwa na Rais Kikwete kuwa
endapo wananchi wataunga
mkono serikali tatu, basi jeshi
litapindua serikali na kuongoza
nchi, au kuleta machafuko nchini.
Mara baada ya uteuzi wa wajumbe
wa Bunge la Maalumu la Katiba,
Mbunge wa Singida Mashariki
ambaye ndiye msemaji katika
suala la katiba na sheria, Lissu,
alinukuliwa akisema:
“Sisi CHADEMA tulisema tangu
mwanzo kuwa tukimuachia Rais
Jakaya Kikwete afanye uteuzi ni
kuhalalisha kupata katiba ya
ubabaishaji, na hili linaashiria
kutokea baada ya wajumbe wa
CCM kuwa wengi kuliko vyama
vingine.”
Alisema wajumbe walioteuliwa
wanaonyesha namna gani
wanavyorudisha asante kwa Rais
Kikwete kutokana na kuteuliwa
katika nafasi hiyo, dalili
inayoonyesha kuwa wajumbe hao
ni watu wake na wataenda
kutekeleza masilahi yake badala
ya wananchi.
Lissu alisema licha ya wajumbe
wengi kuonyesha wazi kuwa na
masilahi na Rais Kikwete,
CHADEMA itapambana kuhakikisha
kuwa katiba inayopatikana
inakuwa kwa masilahi ya
wananchi na si wanasiasa.
Post a Comment