CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema
hakitishiwi nyau kuungana kwa vyama vinne
vya upinzani kwa lengo la kuking’oa
madarakani.Kimesema muungano huo wa
wapinzani si halali na ni sawa na ndoa ya
mkeka.
Pia kimesema ni ndoto za alinacha kwa
wanandoa hao wa msimu, ambao kila mmoja
anatafuta ulaji, kuing’oa CCM, ambayo
imesimamia maendeleo ya nchi pamoja na
kuifanya kuwa na amani na mshikamano.
Kauli hiyo imetolewa jana na Makamu
Mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula,
wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusiana na ndoa hiyo ya wapinzani.
Ndoa hiyo ilifungwa juzi katika viwanja vya
Jangwani, Dar es Salaam, na viongozi wa vyama
hivyo, Freeman Mbowe (CHADEMA), James
Mbatia (NCCR-MAGEUZI), Profesa Ibrahim
Lipumba (CUF) na Emmanuel Makaidi (NLD).
Kwa mujibu wa viongozi hao, makubaliano hayo
yanalenga kuhakikisha wanaing’oa CCM
madarakani katika uchaguzi ujao wa serikali za
mitaa na ule wa rais na wabunge. Pia
kuungana na kuhamasisha wananchi kuipigia
kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, habari za kuaminika zinasema
kuwa, vyama hivyo vimejificha chini ya
mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), ili kukwepa mawimbi makali kutokana
na vyote kukabiliwa na migogoro mizito
inayohatarisha uhai wake.
Mangula alisema takwimu zinaonyesha kuwa
wapinzani hawana uwezo wa kuing’oa CCM,
kwani wamekuwa wakipata asilimia 61 hadi 89
katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani
na kuwaachia wapinzani asilimia chache.
Pia alisema Watanzania wamekuwa wakipigia
kura CCM kutokana na kuvutiwa na sera zake
za maendeleo, amani na mshikamano, tofauti
na wapinzani ambao wamekuwa wakipiga
kelele bila kuonyesha uwajibikaji kwa vitendo.
“Kwa takwimu hizo, maana yake CCM ikipata
asilimia 89 ya kura, vyama vyote vya upinzani
vinagawana asilimia ndogo, hivyo ndoa yao ni
kama ya mkeka na hakuna uhusiano wowote
wa kuishinda CCM,” alisema.
Alitoa mfano wa uchaguzi mkuu wa kwanza
chini ya mfumo wa vyama vingi, ambao CCM
ilishinda kwa asilimia 80, mwaka 2000 asilimia
87 na mwaka 2005 ilishinda kwa asilimia 89
katika kura za wabunge.
Kwa upande wa kura za Rais, mwaka 1995
ilishinda kwa asilimia 61.8, 2000 ilishinda kwa
asilimia 71 na mwaka 2005 CCM ilishinda kwa
asilimia 80.2 huku vyama vyote vikigawana
asilimia 38 mpaka 20.
“Kutokana na hali hiyo, nawatakia kila kheri na
kwamba wakikosa mgombea katika uchaguzi
mkuu wa mwakani, CCM inaweza kuwakopesha
kwa kuwa inao wengi,” alisema.
Mangula alisema muungano huo wa wapinzani
hautapunguza idadi ya mashina wala matawi
ya CCM, hivyo ndoto zao kushika dola
hazitatimia.
Chini ya ndoa hiyo ya mkeka, viongozi hao
walisema watasimamisha mgombea mmoja wa
urais katika uchaguzi wa mwakani na katika
uchaguzi wa serikali za mitaa wa Desemba 14,
mwaka huu, pia vitaungana.
Muungano huo wa vyama vinne vya upinzani
chini ya UKAWA, ulianzia katika Bunge Maalumu
la Katiba, ambapo baadae walisusia vikao hivyo
na hatimaye Bunge liliendelea na kupata
theluthi mbili za wajumbe kwa Bara na
Zanzibar na Katiba Inayopendekezwa kwa
wananchi kupatikana kwa kishindo.
Mangula aonya
Katika hatua nyingine, Mangula amewaonya
viongozi wa CCM wa ngazi za wilaya
kutowagawa wanachama kwa lengo la
kuimarisha makundi yao, badala yake
waimarishe kundi moja la CCM.
Alisema viongozi wa Chama katika wilaya na
mikoa, wakiwemo wabunge na wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wanapaswa
kuhakikisha Chama kinafanya vizuri katika
uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mangula alisema yapo maeneo wabunge na
wajumbe wa NEC wanavutana kwa lengo la
kupanga safu, jambo ambalo alisema kamwe
halitavumiliwa na watakaobainika
wataadhibiwa.
“Wakati huu ni wa kuimarisha kundi moja la
CCM ili iweze kushinda uchaguzi wa serikali za
mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani, lakini si
muda wa kuimarisha kundi la mtu fulani,”
alisema.
Mangula alisema uzoefu unaonyesha kwamba
maeneo ambayo CCM ilishindwa katika
uchaguzi, sababu zilitokana na makundi ndani
ya Chama, hivyo aliwaonya viongozi hao
kuwaachia wanachama waamue.
Alisema amekuwa akifanya ziara na kufuatilia
maendeleo ya Chama katika maeneo
mbalimbali nchini, lakini yapo maeneo ambayo
viongozi hawaelewani kwa sababu ya makundi
yasio na tija kwa Chama.
Mangula alisema CCM inafuatilia kwa kina
maelekezo yake wa viongozi wa mikoa, wilaya,
kata, matawi na mashina na yeyote
atakayebainika kuvuruga uchaguzi huo kwa
sababu za kuimarisha kundi lake, Chama
kitamchukulia hatua.
Akizungumzia mkakati wa Chama katika
uchaguzi huo, Mangula alisema CCM ina
mtandao wa uongozi hadi ngazi ya tawi, ambao
unajisimamia katika mipango yao.
“Tutashinda uchaguzi wa serikali za mitaa na
kwamba hakuna kiongozi wa kitaifa
atakayekwenda kufanya kampeni kwenye
uchaguzi huo. Katika vijiji na mitaa, CCM ina
viongozi wanaoaminika kwa wananchi na ndio
watakaofanya kampeni,” alisema,,
Post a Comment