Mfanya biashara aliyejiuwa kwa risasi jijini arusha chanzo chabainika,tofauti na kusababisha ajali, mahaba niuwe ni sababu kubwa

SAKATA la Mkurugenzi wa Kampuni ya Kitalii ya
DAGT, Timoth Mroki, kujiua kwa kujilipua kwa
risasi, limeibua mambo mapya kutokana na
kuelezwa kuwa wivu wa kimapenzi.
Habari zilizopatikana jijini Arusha, zinasema
kuwa Mroki (36), alikuwa na vimada wawili
ambao ni wake za watu na kuwa kabla ya
kujilipua kwa risasi na kupoteza maisha, alitoa
taarifa kwa wanawake hao (majina
yanahifadhiwa).
Imeelezwa kuwa Mroki alikuwa akitoka na
wanawake hao kila mmoja kwa muda wake,
lakini baadaye siri hiyo ilianza kuvuja na
hatimaye vimada kufahamiana, ikiwa ni pamoja
na mkewe kuanza kupenyezewa taarifa hizo.
Mroki, ambaye pia ni Meneja wa Operesheni na
Masoko wa Kampuni ya Tanzania Bush Camp,
alijiua kwa kujipiga risasi Oktoba 25, mwaka
huu, saa 1:00, baada ya kubaini kuwa vimada
wake hao wamefahamiana.
Habari kutoka kwa mtu wa karibu zimesema
kuwa, vimada hao baada ya kufahamiana,
walikutana na kufanya mazungumzo kisha
kupiga picha pamoja na kumrushia kupitia simu
ya mkononi.
Kugundulika kwa siri hiyo, kulizusha taharuki
kwa Mroki, hivyo kusababisha kuyumba kwa
uhusiano baina yake na vimada hao, akiwemo
mmoja ambaye pia ni mshirika wake
kibiashara.
“Hawa wanawake wana siri nzito kuhusiana na
kifo hiki kwa sababu kabla ya kufanya uamuzi,
aliwasiliana nao…kikubwa awali walikuwa
hawafahamiani ila baadaye walikutana na
kuungana kuwa kitu kimoja.
“Haifahamiki ni kwa vipi walijenga urafiki, ila
watu wa karibu wanasema walijipanga
kumkomoa ili afilisike kwa kuwa kila mmoja
alikuwa na malengo yake,” alisema mtoa habari
wetu.
Kuungana kwa wanawake hao kumlichanganya
Mroki, ambaye tayari uhusiano wake nyumbani
pia ulianza kuwa tete baada ya mkewe kuhisi
kuna mambo yanafanyika kinyume cha
utaratibu.
Hata hivyo, habari zaidi zinasema kuwa
miongoni mwa wanawake hao, yupo aliyejenga
uswahiba na mke wa marehemu huku
uhusiano wa kimapenzi ukifichwa chini ya
mwamvuli wa biashara.
Chanzo chetu kimesema kuwa, kutokana na
ukaribu huo, familia hizo zimekuwa na kawaida
ya kutembeleana, ikiwa ni pamoja na watoto
kukaa kwa siku kadhaa nyumbani kwa kimada
mmoja.
Imeelezwa kuwa kutokana na kugundulika kwa
siri hiyo, Mroki alichukua uamuzi wa kujimaliza
ili kukwepa aibu mbele ya familia.
“Kugonga gari si sababu ya Mroki kujiua, ni
kutokana na kutingwa na mambo mengi
kichwani, hasa baada ya siri ya kimapenzi
kuanza kubainika,” aliongeza mmoja wa rafiki
wa marehemu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus
Sabas, alisema Mroki alijiua kwa kujipiga risasi
kifuani kwa kutumia bastola aina ya KEL –TEC
yenye namba HCB21.
Katika taarifa yake, Kamanda Sabas alisema
kabla ya tukio hilo, Mroki alikuwa na gari
namba T222CMX, aina ya Isuzu Double Cabin,
iliyokuwa ikitokea Mbauda kwenda katikati ya
jiji.
Hata hivyo, taarifa hiyo iliongeza kuwa kutokana
na msongamano wa magari, Mroki alitanua
barabara kukwepa foleni huku akiwa katika
mwendo kasi.
Alipofika maeneo ya Shams, aligongana na gari
la mizigo, mali ya Kampuni ya Gupta, lenye
namba T548 BRL.
Taarifa ilisema pamoja na kusababisha ajali
hiyo, Mroki aliendelea na safari yake ndipo
madereva wa bodaboda walipoamua
kumfukuza na kumkamata eneo la kona ya
Nairobi Ngarenaro.
Mroki aliporejea eneo la tukio na kuulizwa
sababu za kusababisha ajali na kuendelea na
safari, alitoa bastola na kufyatua risasi mbili
hewani na ya tatu kumpiga kifuani.

Post a Comment

Contact Form

Name

Email *

Message *

designed by izack. Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget