MFANYABIASHARA wa Arusha anayemiliki
kampuni ya Tanzania Bush Camp yenye
kambi za watalii katika hifadhi za
Serengeti mkoani Mara na Manyara iliyopo
katika mikoa ya Arusha na Manyara,
Timoth Mroki (36) amejiua kwa kujipiga
risasi tatu kifuani akiwa katika baa
maarufu ya Arusha Raha iliyopo la Shams,
jijini hapa.
Kisa cha kujiua kwake kimetajwa ni
kusababisha ajali, baada ya kuligonga gari
jingine katika eneo la Mbauda wakati
akitokea katika makazi yake yaliyopo eneo
la Kwa Mrombo, jijini hapa.
Alifikwa na mauti katika tukio lililotokea
kati ya saa 1:30 na saa 2:00 usiku, ndani ya
baa maarufu ya Arusha Raha.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo,
Mroki alifika katika baa hiyo baada ya
kufanikiwa kuwatishia kwa risasi
waendesha bodaboda waliokuwa
wamemzingira katika eneo la ajali na
kisha kuondoka kwa kasi kwa gari lake
aina ya Nissan Navara.
“Alipiga risasi mbili hewani waliokuwa
wamemzunguza wakanywea, akatumia
mwanya huo kukimbia na moja kwa moja
akafika Arusha Raha pengine kwa lengo la
kujificha, na hapo akaanza kunywa…
“Ingawa inaonekana alikotoka alikunywa
kidogo, alipofika Arusha Raha alikunywa
haraka pombe mbili kali aina ya Valuer na
wakati anamalizia ya tatu, akajikuta
anazingirwa tena na wale waendesha
bodaboda,” anasema mtoa habari huyo na
kuongeza kuwa, baada ya kufyatua tena
risasi mbili nyingine hewani, lakini bila ya
dalili ya watu hao kutishika, ndipo
akaamua kujimiminia risasi.
Habari zaidi zinasema wakati anazingirwa,
naye akijihami kwa risasi wasamaria wema
wakiwa harakati za kupiga simu polisi
walishitukia polisi wakiingia katika eneo la
tukio lakini tayari Mroki alikuwa
ameshajitoa uhai baada ya kujimiminia
risasi kifuani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha,
Liberatusa Sabas hakupatikana
kuzungumzia tukio hilo, ingawa ofisi ya
Mkuu wa Upelelezi ya wilaya ya Arusha
imekiri kuwepo kwa tukio, lakini chanzo
chetu kikikataa kutajwa jina gazetini kwa
kuwa si wasemaji wa matukio ya jeshi hilo
mkoani Arusha.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika
chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali
ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Post a Comment