WAZUNGU wawili ambao ni mume na mke
wanaodaiwa kuwa ni raia wa Afrika Kusini,
wamekutwa wamekufa chumbani kwao
katika nyumba waliyokuwa wakiishi maeneo
ya Slipway, Masaki jijini Dar es Salaam
Jumatano hii.Chanzo cha kuaminika
kimeeleza kuwa wawili hao ambao walikuwa
wakifanya kazi katika baa iitwayo Mashua
iliyo ndani ya Slipway, huku mwanamke,
aliyetajwa kwa jina la Hotsan, akiwa ndiye
Meneja, walikutwa chumbani kwao wakiwa
wamefariki baada ya kutoonekana kazini
tokea Jumanne, siku ambayo Watanzania
walikuwa wakikumbuka miaka 15 baada ya
kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere.
Inadaiwa kuwa baada ya kutotokea kazini
katika muda wa kawaida, wafanyakazi
wenzao walijaribu kupiga simu zao za
mikononi, lakini zote zilikuwa zikiita pasipo
kupokelewa karibu mchana kutwa na hivyo
kuwapa maswali mengi yasiyo na majibu.
Siku iliyofuata, inadaiwa kuwa wafanyakazi
wenzao walipojaribu tena kupiga namba
hizo, simu zote mbili hazikupatikana.
Awali, walihisi huenda wenzao wameamua
kuacha kazi baada ya kupata sehemu
nyingine, lakini baadaye wakafikia uamuzi
wa kuwafuatilia nyumbani kwao ili kujua
kilichotokea.
Walipofika, walikuta milango ikiwa
imefungwa kwa ndani, kitu kilichowafanya
waamini kuwa walikuwa ndani. Kwa
kushirikiana na majirani, wafanyakazi hao
waliamua kuvunja mlango wa chumba
wanacholala wanandoa hao na kuwakuta
wakiwa kitandani wamelala, kila mmoja
akiwa amegeukia upande wake.
Baada ya kuona tukio hilo la kushtusha,
waliamua kuwaita Polisi ambao walipofika
na kuiona miili hiyo, waliamua kuwaita
wenzao wa kitengo maalum cha uchunguzi
(Crime Investigation) ambao baada ya
kufika, waliwataka raia na majirani
waliokusanyika hapo kukaa mbali ili
kuwapisha kufanya uchunguzi.
Askari hao walikaa na miili ya marehemu
kwa zaidi ya saa tatu wakiwafanyia
uchunguzi na baada ya kukamilika kwa
zoezi hili, miili hiyo ilichukuliwa kupelekwa
hospitalini Muhimbili.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni,
Camillius Wambura alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kuwataja marehemu kuwa ni
Roxxana Hilari na Hainess Hilton William na
kwamba uchunguzi zaidi juu ya kilichowaua
unaendelea.
Post a Comment